MABORESHO YA SHERIA YA ELIMU KUENDANA NA MAGEUZI YA SERA MPYA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

MABORESHO YA SHERIA YA ELIMU KUENDANA NA MAGEUZI YA SERA MPYA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kufanyia maboresho Sheria ya Elimu ili iendane na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na maboresho ya mitaala.

Mhe. Wanu aliyasema hayo jijini Dar es Salaam Februari 13, 2026, alipomuwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, katika kikao cha wadau wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) kilicholenga kutoa maoni kuhusu mapitio ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353.

Amesema utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 unagusa ngazi zote za elimu na mafunzo. Hivyo, Wizara inaendelea na tathmini ya Sheria ya Elimu na sheria za taasisi zilizo chini yake sambamba na mapitio ya miundo ya taasisi hizo kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa sera hiyo.

“Sote tunakubaliana kuwa uwepo wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023 ni jambo moja, lakini utekelezaji wake unahitaji nyenzo mbalimbali.

Mojawapo ni kuwa na Sheria ya Elimu iliyoboreshwa. Tunawashukuru wadau kwa kuendelea kutoa maoni ya kuboresha sheria yetu,” amesema Mhe. Wanu.

Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Martha Makala, amesema mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, Sura ya 353, yanatoa fursa ya kujenga Tanzania yenye elimu jumuishi, yenye ubora na inayolinda haki za watoto na wanafunzi, pamoja na kukabiliana na changamoto ikiwemo ukosefu wa ajira.

Ameipongeza Wizara kwa kushirikisha wadau katika mchakato huo, akibainisha kuwa mtandao huo umetoa maoni katika maeneo yanayohitaji maboresho, ikiwemo suala la wanafunzi wanaokatisha masomo.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa ni kuwepo kwa kifungu kinachoeleza bayana namna ya kuhakikisha wanafunzi waliokatisha masomo wanarejeshwa na kukamilisha mzunguko wao wa elimu. Pia, imependekezwa elimu ya lazima ya miaka 10 iwekwe kisheria, pamoja na elimu bila ada ili kuhakikisha uendelevu wake.

Aidha, wadau wamependekeza suala la lishe shuleni kwa wazazi na walezi liwekwe kisheria ili kuongeza uwajibikaji, pamoja na kufanya marekebisho ya sheria ili kuondoa ukinzani uliopo kati ya Sheria ya Ndoa na sheria ya elimu, na kuhakikisha uendelevu wa Bodi ya Kitaaluma ya Walimu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, Prof. Saudin Mwakaje, amesema mapitio hayo yanalenga kuimarisha mifumo ya kijamii na kiuchumi na kukidhi mahitaji ya mabadiliko mapya, hususan katika utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Wakichangia maoni yao, wadau wameiomba Wizara kuangalia upya muda wa masomo ya ziada (tuition), wakieleza kuwa baadhi ya walimu hutumia vipindi hivyo kufundisha mada zinazopaswa kufundishwa darasani, hali inayowaathiri wanafunzi wasioweza kuhudhuria vipindi hivyo.

Pia wamependekeza lugha ya alama ifundishwe kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kurahisisha mawasiliano, hususan katika huduma za jamii kama hospitali na masoko.

Kadhalika, wadau wamependekeza shule mpya za sekondari zinazojengwa nchini ziwe na mabweni, hatua itakayosaidia kulinda watoto wa kike dhidi ya vishawishi na kuongeza usalama pamoja na ufanisi wao katika masomo.

No comments:

Post a Comment