NMB YADHAMINI MAONESHO YA TRI-NATIONS LIVESTOCK EXPO KWA SHILINGI MILIONI 300, SERIKALI YAIPONGEZA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

NMB YADHAMINI MAONESHO YA TRI-NATIONS LIVESTOCK EXPO KWA SHILINGI MILIONI 300, SERIKALI YAIPONGEZA


Benki ya NMB Bank Plc imesaini makubaliano ya udhamini wa miaka mitatu yenye thamani ya Shilingi milioni 300 kwa ajili ya Maonesho ya Kimataifa ya Mifugo ya Tri-Nations Livestock Expo yatakayofanyika kuanzia mwaka 2026 hadi 2028.


Maonesho hayo, yanayowakutanisha wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo kutoka Tanzania, Kenya na Namibia, yatafanyika kuanzia Juni 19 hadi 21 mwaka huu katika viwanja vya Ubena Zomozi, Chalinze mkoani Pwani.


Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Nsolo Mlozi, alisema benki hiyo imeamua kuwekeza kimkakati katika maonesho hayo kufuatia mafanikio yaliyopatikana katika miaka miwili iliyopita ya 2024 na 2025.


“Mkataba huu ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kukuza sekta ya ufugaji na kuboresha maisha ya Watanzania wanaojishughulisha na sekta ya kilimo kwa ujumla, ikiwemo mnyororo wa thamani unaohusisha kilimo, uvuvi na ufugaji,” alisema Mlozi.


Alibainisha kuwa hadi kufikia mwaka 2025, NMB ilikuwa imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 100 kwa ajili ya sekta ya kilimo, hatua inayodhihirisha dhamira ya benki hiyo katika kuiendeleza sekta hiyo muhimu ya uchumi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mbogo Ranches, Naweed Bulla, aliishukuru NMB kwa kukubali kudhamini maonesho hayo, akisema mchango huo utaongeza hadhi na mafanikio ya tukio hilo la kimataifa.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Fabian Madele, alipongeza ushirikiano huo akieleza kuwa utaimarisha zaidi maonesho hayo pamoja na kukuza sekta ya mifugo nchini. Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wa mkataba huo wa miaka mitatu.


Maonesho ya Tri-Nations Livestock Expo ni jukwaa la kimataifa linalolenga kuimarisha ushirikiano, ubunifu na fursa za kibiashara kwa wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo. Kupitia maonesho hayo, washiriki hupata elimu ya mbinu bora za ufugaji, huduma za bima, fursa za mikopo pamoja na masoko ya kitaifa na kimataifa.


Udhamini huo wa NMB unatarajiwa kuongeza thamani ya maonesho hayo na kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo, ambayo ni muhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi wa Tanzania.



Mwisho*

No comments:

Post a Comment