WABUNIFU 3,000 WATAMBULIWA KUPITIA MFUKO WA SAMIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

WABUNIFU 3,000 WATAMBULIWA KUPITIA MFUKO WA SAMIA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema Serikali ilitenga dola za Marekani milioni moja, sawa na shilingi bilioni 2.3, kwa ajili ya kutoa mitaji wezeshi kwa kazi bunifu kupitia Mfuko wa Samia unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Amesema mfuko huo uliozinduliwa Novemba 2024 ni mwendelezo wa juhudi za makusudi za Serikali za kuimarisha sekta ya ubunifu. Amebainisha kuwa hadi sasa Wizara imefanikiwa kuwatambua zaidi ya wabunifu 3,000 kote nchini.

Naibu Waziri ameyasema hayo leo Februari 13, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla iliyofanyika COSTECH kwa ajili ya kuwapongeza vijana walionufaika na mitaji hiyo ili kuendeleza bunifu zao.

Ameeleza kuwa wabunifu hao walitambuliwa kupitia mashindano ya MAKISATU, na kwamba kutokana na wingi wa wabunifu nchini, Serikali ya Awamu ya Sita imeielekeza COSTECH kuwasaidia wabunifu, hususan vijana, kukabiliana na changamoto za ushindani sokoni.

Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unalenga kuwawezesha Watanzania wenye kazi bunifu wanaokabiliwa na vikwazo vya kuingiza bidhaa zao sokoni.

“Kama mnavyokumbuka, tarehe 27 Februari 2025 tulikutana katika tukio la kutia saini makubaliano kati ya COSTECH na CRDB Bank kwa lengo la kuendeleza jukumu hili la kuwezesha wabunifu,” amesema.

Amefafanua kuwa makubaliano hayo yalihusisha Serikali kuwekeza CRDB shilingi bilioni 2.3 kutoka kwenye mfuko, huku CRDB nao wakiwekeza mtaji wa shilingi bilioni 2.3, na hivyo kufanya mfuko huo kuwa na jumla ya shilingi bilioni 4.6.

Aidha, amewapongeza wabunifu walionufaika na mfuko huo, akitaja mfano wa kijana aliyeongeza thamani kwenye mazao ya asali na nyuki na kufanikiwa kusafirisha nje ya nchi zaidi ya tani 60.

Amesema kijana huyo ameweza kukuza biashara iliyofikia thamani ya shilingi milioni 200, huku mbunifu mwingine akiwekeza katika biashara ya miti mkoani Morogoro na Mkoa wa Pwani.

Hata hivyo, Naibu Waziri ameonesha masikitiko yake kuhusu kasi ndogo ya uchukuaji wa mikopo kupitia mfuko huo.

“Pamoja na habari njema, nimesikitishwa na kasi ndogo ya uchukuaji wa mikopo. Nimeambiwa katika miezi 10 vijana saba tu wamefanikiwa kunufaika na Mfuko wa Samia. Hadi sasa ni shilingi milioni 700 tu zimechukuliwa kati ya bilioni 4.6,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na idadi kubwa ya wabunifu nchini, matarajio yalikuwa fedha hizo zingechukuliwa ndani ya mwaka mmoja. 

Amesema watendaji wa COSTECH na CRDB wameeleza changamoto mbalimbali zinazosababisha waombaji kukwama.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amesema mfuko huu ni fedha inayozunguka (revolving fund) ambapo vijana wakopeshwe, warejeshe na wengine wanufaike na kuwa Mfuko unalenga kuhamasisha uchumi wa ubunifu, kuongeza ajira na kuhakikisha bunifu za vijana zinageuka kuwa biashara endelevu na viwanda vinavyochangia pato la taifa, huku COSTECH ikiendelea kuwajengea uwezo vijana na kuwasaidia katika masuala ya viwango, vibali na uratibu wa kiserikali.


No comments:

Post a Comment