Na Mwandishi Wetu (Kigoma
Imeelezwa kuwa Mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 9,009 Awamu ya Pili B (HEP 2B) utakaonufaisha Wateja wa awali 290,300 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara nchini unakwenda kuchochea shughuli za kiuchumi, Biashara na Viwanda na kuongeza Pato la Taifa.
Hayo yameelezwa leo Februari 13, 2026 na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Bw. Abbas Rugwa wakati akitambulishwa mkandarasi kampuni ya Silo Power Ltd atakayetekeleza mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 196 kwa gharama ya shilingi bilioni 39.7 mkoani Kigoma.
"Nimeelezwa kuwa, mradi wa HEP 2B unakwenda kuunganisha wateja wapatao 6,308. Hii inakwenda kuchochea maendeleo ya wakazi wa mkoa huu kuweza kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kufungua Viwanda na Biashara, " Amesema Bw. Rugwa
Halikadhalika, Bw. Rugwa amemtaka mkandarasi kuhakikisha anamaliza mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vitongoji kwa muda uliopangwa ili wananchi wa mkoa huo waweze kunufaika na mradi ikiwemo kufungua shughuli za kibiashara.
Naye, Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi Mhandisi Robert Dulle ameeleza kuwa, kwa mkoa wa Kigoma jumla una vijiji 306 ambavyo vyote vina huduma ya umeme. Aidha, Mha. Dulle ameongeza kuwa katika mradi wa HEP 2B unakwenda kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote visivyokuwa na umeme katika Mkoa wa Kigoma.





No comments:
Post a Comment