MKURUGENZI IAEA AIPONGEZA SERIKALI NA BMH KWA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA SEKTA YA AFYA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 3, 2026

MKURUGENZI IAEA AIPONGEZA SERIKALI NA BMH KWA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA SEKTA YA AFYA




Na Jeremia Mwakyoma-DODOMA


Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic (IAEA) Kanda ya Afrika Bw. Gashaw Molde ameipongeza Serikali ya Tanzania na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa uwekezaji mkubwa ilioufanya katika Sekta ya Afya ikiwemo kuendelea kuimarisha eneo la huduma za matibabu ya ugonjwa wa Saratani.

Akitembelea ujenzi wa mradi wa kituo cha Umahiri cha Mafunzo na Matibabu ya Saratani kinachojengwa BMH, Bw. Welde amesema kuwa kituo hicho kitakapokamilika na uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Afya kutaifanya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha matibabu (Medical Hub) kwa nchi za jirani zinazozunguka Tanzania.

"Tanzania itakuwa kituo cha matibabu kinachotegemewa siyo tu na Watanzania bali hata na Mataifa yanayoizunguka Tanzania; uwekezaji katika Sekta ya Afya nchini Tanzania kunaiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika kukuza Tiba Utalii " alisisitiza Bw. Welde.

Aliongeza kuwa Tanzania ni mshirika muhimu wa IAEA hivyo ushirikiano uliopo utaimarika zaidi na amejionea utashi na utayari Mkubwa wa Serikali ya Tanzania kuwekeza katika huduma za matibabu ya ugonjwa wa Saratani, hivyo IAEA inaunga mkono programu za Tanzania za huduma za Saratani ikiwemo kutoa mafunzo kwa Wataalamu na kusaidia upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa vya teknolojia ya juu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Dkt. Henry Humba amesema kuwa Serikali ya Tanzania imefanya mapinduzi makubwa kwenye Sekta ya Afya, inaendelea kuimarisha huduma za matibabu ya Saratani kwa kujenga mradi mkubwa wa Kituo cha mafunzo na matibabu ya Saratani hapo BMH ambapo ujenzi umefika asilimia 61% na utagharimu shilingi Bil. 30.4 huku ukitarajiwa kukamilika Agosti 2026.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania (TAEC) Prof. Najat Mohaned amesema kuwa TAEC watahakikisha kituo hicho cha Saratani cha BMH kitakuwa kituo salama katika utoaji wa huduma za matibabu ya saratani na kuwa TAEC itaendelea kushirikiana na BMH kwa karibu.

Akimuwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma na Utafiti Prof. Razack Lokina amesema kuwa UDOM ni mshirika mkubwa wa BMH, kwa pamoja watatumia kituo hicho kuzalisha Wataalamu wa kutosha wa utoaji tiba za Saratani, kufanya tafiti zitakazosaidia kuboresha mipango na mikakati ya nchi katika kushughulikia tatizo la Saratani ikiwemo Mkakati wa Taifa wa kupambana na Ugonjwa wa Saratani.

No comments:

Post a Comment