MRADI WA SINYA-NAMANGA KUWA SULUHU YA HUDUMA YA MAJI LONGIDO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, February 23, 2026

MRADI WA SINYA-NAMANGA KUWA SULUHU YA HUDUMA YA MAJI LONGIDO


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) amesema Mradi wa Maji wa Sinya-Namanga utakuwa ni suluhu ya changamoto ya muda mrefu ya huduma ya maji kwa wananchi wa Longido.

Ametoa kauli hiyo mara baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika Kijiji cha Ildonyo, Kata ya Sinya, wilayani Longido katika Mkoa wa Arusha.

“Serikali yenu inajali wananchi wake kwa kutoa majawabu ya kero zao ndio maana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza kipatikane chanzo cha maji mahali popote na maji yake yafike kwa wananchi hawa kwa gharama yoyote”, Waziri Mkuu amesema.

Dkt. Nchemba amesema kwa miaka mingi Wilaya ya Longido imekuwa na changamoto kubwa ya maji, lakini Mradi wa Maji wa Sinya- Namanga unakwenda kumaliza changamoto hiyo.

“Hii inadhihirisha jinsi Serikali yenu inavyotoa majawabu kwa wananchi wake, nyinyi ni sehemu ya mashahidi kupitia utekelezaji wa mradi huu mkubwa”, Dkt. Nchemba amesema.

Ameongeza kuwa maji ni hitaji la msingi kwa wakazi wa Longido kwa ajili ya binadamu, wanyama na shughuli za kila siku, ndio maana Serikali ikachukua hatua kuwekeza takribanj Sh. bilioni 13.5 kutekeleza mradi huo.

Aidha, Dkt. Nchemba ametoa rai kwa wakazi wa Longido kuilinda na kutunza miundombinu ya maji kwa kutokukata mabomba ili mradi uwe endelevu na kutoa huduma bora kwa miaka mingi ijayo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema lengo la mradi ni kumaliza tatizo la upungufu wa huduma ya majisafi katika Kata za Namanga na Sinya, ambazo kimsingi kuna changamoto ya vyanzo vya maji.

Amebainisha kuwa mradi huo umetokana na ongezeko la watu na mahitaji makubwa ya maji katika maeneo hayo.

Ambapo kwa sasa, chanzo cha mradi huo cha Mto Simba kilichopo Siha, mkoani Kilimanjaro, kinazalisha lita 1,700,000 kwa siku, huku mahitaji halisi yakiwa lita 3,800,000 kwa siku, hali inayosababisha upungufu mkubwa wa majisafi kwa wananchi.

Amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) ilichimba kisima kirefu katika eneo la Ildonyo, Sinya chenye uwezo wa kuzalisha lita 2,400,000 kwa siku.

Baada ya mradi kukamilika, uzalishaji wa maji unatarajiwa kufikia lita 4,100,000 kwa siku, kiwango kitakachokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Akitoa taarifa ya mradi, Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Justin Rujomba ameeleza kuwa miongoni mwa kazi zilizofanyika ni pamoja na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba ya usambazaji kwa kilomita 9.5 katika Kata ya Sinya.

Uekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Aprili, 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2027. Hadi sasa, utekelezaji umefikia asilimia 25. Mradi unatekelezwa na Mkandarasi mzawa, M/s Zongii Contractors Co. LTD kutoka Mwanza.

Kukamilika kwa mradi huo kutamaliza kilio cha upatikanaji wa majisafi kwa wananchi wa Namanga na Kimokouwa.




No comments:

Post a Comment