NeST KUONDOA UCHELEWESHAJI WA MALIPO KWA WAZABUNI - PPRA YAIHAKIKISHIA KAMATI YA BUNGE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 24, 2026

NeST KUONDOA UCHELEWESHAJI WA MALIPO KWA WAZABUNI - PPRA YAIHAKIKISHIA KAMATI YA BUNGE


Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefanya wasilisho kuhusu maendeleo ya usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, aliieleza Kamati hiyo kuwa Mfumo wa NeST unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya ucheleweshaji wa malipo kwa wazabuni, kufuatia kuunganishwa kwake na mifumo ya malipo na mifumo ya bajeti ya Serikali.

Bw. Simba alieleza kuwa hadi sasa Mfumo wa NeST una moduli sita kuu, ambazo ni Moduli ya Usajili, Moduli ya Uchakataji wa Zabuni, Moduli ya Usimamizi wa Mikataba, Moduli ya Upokeaji wa Malalamiko, Moduli ya Mnada wa Kielektroniki, pamoja na Moduli ya Malipo ya Kielektroniki (e-payment).

“Kupitia moduli ya malipo ya kielektroniki, taasisi nunuzi zinaweza kutekeleza michakato yote ya zabuni kupitia Mfumo wa NeST hadi hatua ya malipo. Mfumo huu umeunganishwa na mifumo ya malipo ya Serikali (MUSE na EMRS).

Aidha, tunakamilisha taratibu za kuunganisha na mifumo ya bajeti. Baada ya kupata kibali cha Serikali, taasisi haitaruhusiwa kuanzisha mchakato wa ununuzi bila kuwa na kifungu cha bajeti husika na kukizuia kwenye Mfumo wa NeST mara tu mchakato unapoanza,” alisema Bw. Simba.

Alifafanua kuwa ucheleweshaji wa malipo kwa wazabuni mara nyingi husababishwa na baadhi ya watumishi wa umma kuanzisha michakato ya ununuzi bila kuhakikisha upatikanaji na ulinzi wa vifungu vya bajeti husika. 

Ameongeza kuwa baadhi ya taasisi nunuzi hubadili matumizi ya vifungu hivyo wakati mchakato ukiendelea, hali inayosababisha changamoto wakati wa kulipa wazabuni.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kutakuwepo dirisha maalum la ununuzi wa dharura kwa zabuni zitakazothibitishwa kuhitaji kuanza mara moja, hata kama hazikupangwa awali katika bajeti ya ununuzi.

“Pamoja na kwamba ucheleweshwaji wa malipo unawaumiza wazabuni, pia unaongeza mzigo wa gharama zisizo za lazima kwa Serikali kwani wazabuni huweka ongezeko kwenye madai (interest rate),” alisema. 

Katika hatua nyingine, Bw. Simba aliieleza Kamati kuwa PPRA imeendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kwenye michakato ya zabuni kwa kuongeza ufanisi wa usimamizi kupitia Mfumo wa NeST. 

Alisema kuwa kuanzia mwezi Machi, mfumo huo utaanza kutuma taarifa za tahadhari (red flag notifications) kwa zabuni zitakazobainika kuwa na viashiria vya ukiukwaji wa taratibu.

 Hatua hiyo itawezesha PPRA kuingilia kati michakato ya zabuni mapema na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusubiri ukaguzi baada ya mchakato kukamilika.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mhe. Khalfan Aeshi, aliipongeza PPRA kwa kuimarisha usimamizi wa ununuzi wa umma kupitia Mfumo wa NeST, na kuisisitiza Mamlaka kuendelea kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kwa umma ili Watanzania wengi zaidi waweze kufahamu na kunufaika na fursa zilizopo.

Alitolea mfano wa asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa umma iliyotengwa kwa ajili ya makundi maalu (vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu), kuwa utekelezaji madhubuti wa mpango huo unaweza kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira na kazi nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Prof. Leonada Mwagike, aliishukuru Kamati kwa maelekezo na ushauri wake, na kuahidi kuyafanyia kazi kwa haraka ili kuendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma nchini.

No comments:

Post a Comment