NMB YAWEZESHA VIJANA 100 KUPITIA MAFUNZO YA KITAALUMA YA BENKI UDSM - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 24, 2026

NMB YAWEZESHA VIJANA 100 KUPITIA MAFUNZO YA KITAALUMA YA BENKI UDSM



Benki ya NMB Bank Plc imeendeleza jitihada zake za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa ya kisasa katika sekta ya fedha nchini kwa kusaidia mafunzo ya kitaaluma na kutalaamu kwa vijana 100 kupitia mpango maalumu wa Graduate Banker Readiness Programme (GBRP) unaotekelezwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). 

Kupitia ushirikiano huo, washiriki wanapatiwa mafunzo ya kinadharia na vitendo yanayolenga kuwaandaa kuingia moja kwa moja katika mazingira halisi ya kazi za benki na taasisi za kifedha.

Kundi la nne la wanufaika wa mpango huo limehitimu Ijumaa iliyopita baada ya kukamilisha mafunzo yaliyowajengea uwezo katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo uchambuzi wa kifedha, uendeshaji wa benki, usimamizi na udhibiti wa vihatarishi, uzingatiaji wa kanuni, utoaji bora wa huduma kwa wateja pamoja na mifumo ya benki ya kidijitali. 

Akizungumza kabla ya kuwakabidhi wahitimu vyeti, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa NMB, Bi. Erica Hanson, alisema mpango huo ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya benki hiyo na UDSM kupitia Shule ya Biashara ya chuo hicho, ukiwa na lengo la kuunganisha elimu ya darasani na uhalisia wa soko la ajira katika sekta ya fedha.

Bi. Hanson alieleza kuwa kuhitimu kwa vijana hao kunaimarisha dhamira ya NMB ya kuendelea kuwa mwajiri pendwa nchini, akibainisha kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji wa makusudi katika kukuza vipaji na rasilimali watu kwa maendeleo endelevu. 

Kwa upande wao, wanataaluma wa UDSM wakiongozwa na Mkuu wa Kitivo cha Biashara, Prof. Omari Mbura, walisema mpango huo unasaidia kupunguza pengo la ujuzi sokoni kwa kuhakikisha wahitimu wanakidhi mahitaji halisi ya tasnia ya fedha. 

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mratibu wa mafunzo kutoka Kituo cha Utafiti wa Benki na Huduma za Kifedha (CBFSR), Prof. Esther Ishengoma pamoja na Mkuu wa Idara ya Fedha, Dkt. Thobias Swai, waliobainisha kuwa programu hiyo imekuwa chachu ya kuandaa wataalamu wenye ushindani.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Marcelina Evarist aliishukuru NMB kwa kuuwezesha mpango huo uliowajengea uwezo, maarifa na uelewa mpana wa sekta ya fedha, akieleza kuwa mafunzo hayo yamewaandaa vyema kukabiliana na changamoto na fursa zilizopo katika tasnia ya benki na huduma za kifedha nchini.




No comments:

Post a Comment