
Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 4,2026 jijini Dodoma kufuatia video iliyoenea mitandaoni ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Mariana Eric Mirindima wa Shule ya Sekondari Jangwani, aliyewasilisha barua ya kueleza changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wanapotumia daladala.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameielekeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuharakisha usajili na uthibitishaji wa madereva na makondakta wa daladala, kuimarisha udhibiti wa nauli za wanafunzi, pamoja na kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya mabasi ya mijini ili kudhibiti vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanafunzi.
Prof. Mbarawa ametoa maelekezo hayo leo Februari 4, 2026 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kusambaa kwa video mitandaoni ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Mariana Eric Mirindima wa Shule ya Sekondari Jangwani, aliyewasilisha barua akieleza changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wanapotumia usafiri wa daladala.
Amesema Serikali haitavumilia vitendo vya baadhi ya makondakta na madereva kuwanyanyasa wanafunzi kwa kisingizio cha kutolipa nauli kamili, akisisitiza kuwa haki ya mwanafunzi kupata elimu kwa usalama haiwezi kuvunjwa kwa maslahi ya kibiashara.
Katika barua yake, mwanafunzi huyo alieleza kuwa baadhi ya makondakta wamekuwa wakigoma kuwabeba wanafunzi, hali inayowasababisha kusimama vituoni kwa muda mrefu, kuchelewa kufika shuleni au kushindwa kabisa kuhudhuria masomo, jambo linalohatarisha usalama wao na kuathiri maendeleo yao ya kitaaluma.
Prof. Mbarawa amempongeza mwanafunzi huyo pamoja na mzazi wake kwa ujasiri wa kutoa taarifa, akieleza kuwa Serikali imeisikiliza sauti ya wanafunzi na itachukua hatua stahiki.
“Kwa kufanya hivyo, mwanafunzi huyu ametimiza wajibu wake wa msingi wa kuipa Serikali mrejesho unaopaswa kufanyiwa kazi. Napenda kuwahakikishia kuwa sauti ya wanafunzi imesikilizwa,” amesema Prof. Mbarawa.
Amefafanua kuwa Serikali imetoa fursa kwa sekta binafsi kutoa huduma za usafiri wa umma, lakini haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watoa huduma watakaokiuka Sheria, Kanuni na staha ya utoaji huduma kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Waziri amesema Serikali imeweka mikakati ya kuboresha usafiri wa wanafunzi mijini ikiwemo kuanzisha mabasi maalumu yaendayo haraka kwa ajili ya wanafunzi nyakati za asubuhi na jioni, pamoja na kutenga mabehewa maalumu ya wanafunzi kwenye treni za mijini, hususan jijini Dar es Salaam.
Aidha, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa nauli maalumu ya Shilingi 200 kwa wanafunzi katika daladala na mabasi yaendayo haraka, pamoja na kutoa elimu kwa watoa huduma na watumia huduma ili kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika sekta ya usafiri wa umma.
Serikali pia imewahimiza wananchi kushiriki katika kuwalinda wanafunzi kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki zao kupitia namba za bure za LATRA au WhatsApp, ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Prof. Mbarawa ametoa onyo kwa wamiliki wa daladala kuhakikisha watumishi wao wanazingatia Sheria na Kanuni, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuwanyanyasa wanafunzi.
Hatua hizi, Serikali imesema, zinalenga kujenga mfumo wa usafiri wa umma unaolinda haki, usalama na ustawi wa wanafunzi ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira salama, yenye heshima na staha.

No comments:
Post a Comment