PROF. MBARAWA: RELI, BANDARI NA USAFIRI WA ANGA VIMEIMARIKA NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, February 1, 2026

PROF. MBARAWA: RELI, BANDARI NA USAFIRI WA ANGA VIMEIMARIKA NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS SAMIA




Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili, sekta ya uchukuzi imepata mafanikio makubwa yaliyoimarisha reli, bandari, usafiri wa majini na anga, hatua iliyoongeza ufanisi wa usafirishaji, usalama wa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo, Februari 1, 2026 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari , kuelezea utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100.

Amesema kipaumbele cha Serikali katika sekta ya uchukuzi ni kulinda maisha ya wananchi na mali zao, hususan katika usafiri wa majini, kupitia kuimarisha mifumo ya utafutaji na uokoaji.

Ameeleza kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Kuratibu Utafutaji na Uokoaji cha Kikanda (Maritime Rescue Coordination Centre – MRCC) katika Ziwa Victoria, Mwanza, ambacho kimeboreshwa kwa mifumo ya kisasa ya mawasiliano, TEHAMA na vifaa vya uokoaji.

“Lengo ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayepoteza maisha wakati akijitafutia riziki ndani ya maji, na endapo ajali itatokea, kuwepo mifumo ya haraka na madhubuti ya uokoaji,” amesema Prof. Mbarawa.

Akizungumzia usafiri wa reli, Prof. Mbarawa amesema Serikali imefanikiwa kufufua Reli ya TAZARA baada ya kukamilisha majadiliano na kusaini mkataba wa ufufuaji na uboreshaji mkubwa wa reli hiyo tarehe 29 Septemba, 2025 baina ya Serikali za Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na Kampuni ya CCECC ya China. Hatua hiyo itaongeza uwezo wa reli na kuimarisha biashara na uunganishwaji wa kikanda, hususan na nchi za Kusini mwa Afrika.

Kwa upande wa reli za ndani, amesema Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa reli za kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma, huku Shirika la Reli Tanzania (TRC) likianza kujitegemea kifedha.

Aidha, uendeshaji wa reli za SGR na MGR umeendelea kuimarika kwa kusafirisha idadi kubwa ya abiria na mizigo, wakati ujenzi wa reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ukiendelea, na kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma kikiendelea kutoa huduma kwa ufanisi
Kuhusu bandari na usafiri wa maji ni.

Prof. Mbarawa amesema Serikali imekamilisha maandalizi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, kuanza maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, pamoja na kuendelea kutekeleza miradi ya bandari katika Maziwa Makuu na ukanda wa Bahari ya Hindi.

Ameongeza kuwa meli mpya za mizigo na abiria zimekamilika na kuanza kutoa huduma, jambo lililoongeza uwezo wa usafirishaji wa majini.

Katika kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, amesema Serikali pia imenunua boti za uokoaji pamoja na vifaa vya huduma za afya kwa ajili ya kukabiliana na dharura na kulinda maisha ya wananchi wanaotumia maji kama chanzo cha usafiri na riziki.

Kwa upande wa usafiri wa anga, Prof. Mbarawa amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa Jengo la Viongozi katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), kuanza maandalizi ya ujenzi wa viwanja vipya vya ndege nchini, pamoja na kupanua wigo wa safari za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), hatua iliyoongeza uunganishwaji wa Tanzania ndani na nje ya nchi.

Asema kuwa mafanikio ya siku 100 katika sekta ya uchukuzi ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuijenga Tanzania yenye miundombinu ya kisasa, salama na yenye tija.

“Miradi ya reli, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini imefikia hatua nzuri za utekelezaji, uwezo wa bandari na usalama wa majini umeimarishwa, na uunganishwaji wa kikanda na kimataifa umeongezeka. Sekta ya uchukuzi itaendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa,” amesema.

No comments:

Post a Comment