Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi,akizungumza na wadau leo Februari 02, 2026 jijini Dodoma.
....
Serikali imeelekeza wadau kuhakikisha uwekezaji unaofanyika karibu na kampasi mpya 16 za vyuo vikuu unazingatia mpangilio wa miji, usalama na viwango vya kitaifa ili kuzuia ujenzi holela na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wanafunzi, watumishi na jamii jirani.
Akizungumza Februari 02, 2026 jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi,amesema kuwa halmashauri na serikali za mitaa zinapaswa kutenga ardhi na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na vyuo husika.
Prof. Mushi amesisitiza kuwa mipango hiyo lazima izingatie viwango vya kitaifa vya upangaji miji na kuondoa migongano ya matumizi ya ardhi.
Profesa Mushi pia amevielekeza vyuo vikuu kufungua milango ya ushirikiano na sekta binafsi kupitia ubia rasmi (PPP) katika ujenzi wa hosteli, vituo vya biashara na miundombinu maalum.
Amesema mashauriano ya mara kwa mara kati ya vyuo na serikali za mitaa ni muhimu ili kuoanisha mipango ya maendeleo na kuimarisha mazingira rafiki kwa uwekezaji.
Aidha, sekta binafsi imetakiwa kuhakikisha huduma wanazotoa zinajibu mahitaji halisi ya jamii kwa kuzingatia usalama, ubora na uwajibikaji wa kijamii.
Mratibu wa Mradi wa HEET Taifa, Dkt. Kenneth Hosea, amesema kuwa mbali na kutoa mafunzo ya programu za Shahada ya Kwanza na Shahada ya Pili, kampasi mpya pia zitalenga kutoa ujuzi wa vitendo kwa vijana, wanawake na makundi maalum. Hatua hii inalenga kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo ya pembezoni kupitia ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa huduma za msingi pamoja na fursa za ajira.
Aidha, Dkt. Hosea ameongeza kuwa kila kampasi inatarajiwa kudahili zaidi ya wanafunzi 1,000 mwanzoni, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia takribani wanafunzi 7,000 kadri muda unavyosonga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga, Rashid Karim Gembe, amesema kuwa kuanzishwa kwa kampasi mpya za elimu ya juu katika maeneo ya pembezoni kumeleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii
Amesema kuwa kutachochea ujenzi wa miundombinu kama barabara, maji na umeme, kuongeza upatikanaji wa huduma za msingi, pamoja na kutoa fursa za ajira kwa wananchi kupitia mahitaji ya walimu, wanafunzi na sekta binafsi, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi wa eneo husika.

No comments:
Post a Comment