
Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya Shingi Bilioni 28 zilizorejesha tabasamu kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ambazo zimetumika kujenga Soko Jipya la Kariakoo na kukarabati Soko la zamani la Kariakoo ambalo liliharibika kutokana na janga la moto Oktoba 07, 2021.

Prof. Shemdoe ametoa shukrani hizo leo kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akitoa neno la utangulizi, wakati ya hafla ya ufunguzi wa Soko Kuu Jipya la Kariakoo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Mhe. Rais natumia fursa hii kutoa shukrani za dhati kwa nia yako njema ya kurejesha tabasamu kwa wafanyabishara na wananchi, kwa kutoa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 28 ili kujenga soko jipya na kukarabati lililoteketea kwa janga la moto la Oktoba 07, 2021”, ameeleza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, Soko la Kariakoo ni kitovu cha biashara ndani ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla, hivyo ofisi yake kwa kutambua hilo itahakikisha soko hilo linatoa huduma bora na kwa ufanisi ili kuleta tija na kuakisi thamani ya fedha iliyowekezwa na Serikali.
Sanjali na hilo, Prof. Shemdoe amesema kuwa, Serikali inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha barabara zote zinazozunguka Soko la Karikakoo na maeneo jirani zinafunguliwa ili ziweze kupitika wakati wote na kulifanya soko litoe huduma kwa wananchi masaa 24.
Aidha, Prof. Shemdoe ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteu kuwa Waziri anayesimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kumuahidi Mhe. Rais kwamba atafanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa.





No comments:
Post a Comment