
Na OWM - TAMISEMI, Colombia
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema ili mageuzi ya uchumi wa vijijini yawe na tija na manufaa kwa wananchi yanapaswa kuhusisha uchumi wa buluu, ufugaji pamoja na misitu na mazao yake.
Prof. Shemdoe amesema hayo Februari 26, 2026 wakati akichangia mada juu ya mageuzi ya uchumi na maendeleo vijijini kwenye mkutano wa pili wa Kimataifa wa Mageuzi ya Uchumi na Maendeleo Vijijini unaoendelea katika mji wa Cartagena, nchini Colombia, akimwakilisha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo.
Mchango huo wa Prof. Shemdoe umelenga kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukifanya kilimo na ufugaji kuwa na faida kwa wananchi na sio shughuli za kujikimu, kukuza uchumi wa bluu kwa kutumia rasilimali za maji kuongeza kipato cha jamii za Pwani, ikiwa ni pamoja na kuhifadhi na kutumia misitu kwa njia endelevu ili kuongeza thamani ya mazao yake na kulinda mazingira.
Katika kikao cha kujadili maazimio ya Mkutano huo, Prof. Shemdoe amesisitiza kutambua shughuli za ufugaji na uvuvi kama sehemu kubwa inayochangia maendeleo vijijini na kuongeza kuwa, kuwe na mkakati kutathmini utekelezaji wa maazimio kwa wakati ili tathmini isifanyike baada ya mikaka 20 kama ilivyofanyika ya mkutano wa kwanza wa mwaka 2006 katika mkutano huu wa pili wa mwaka 2026.
Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe ameongoza ujumbe wa Tanzania kufanya kikao cha pembeni cha uwili kati ya Tanzania na Indonesia ambapo ujumbe wa Indonesia uliongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Ir. Sam Herodian.
Katika kikao hicho, Tanzania na Indonesia zimejadiliana kufufua ushirikiano wao kwenye njanja za kilimo cha mpunga na ufadhili wa masomo kwa Watanzania nchini Indonesia kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Majadiliano yetu yamepelekea tuanze maandalizi ya rasimu ya hati ya makubaliano kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ubalozi wa Indonesia nchini Tanzania,” amesema Prof. Shemdoe.
Vile vile, Prof. Shemdoe amekutana na kufanya mazungumzo na Amy Regas, Mwakilishi wa Shirika la Land Facility ambalo limeonesha nia ya kuifadhili TAMISEMI kuandaa mradi mkubwa wa kujengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, biashara ya kaboni kupitia Mkutano wa Wadau wa Maendeleo (Donor Roundtable meeting) utakaofanyika mwezi Mei, 2026.




No comments:
Post a Comment