RC Sendiga Ataka Heshima na Uwajibikaji Ndani ya Ndoa - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 6, 2026

RC Sendiga Ataka Heshima na Uwajibikaji Ndani ya Ndoa


Manyara — Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, amewataka wanawake wakiwemo viongozi kutambua na kuheshimu nafasi zao ndani ya ndoa, akisisitiza kuwa mwanamke kufahamu haki zake hakumaanishi kumpunguzia heshima mumewe, kwani wanaume nao wanahitaji kutunzwa na kuheshimiwa.

RC Sendiga ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Manyara, katika mwendelezo wa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM, ambapo pia alibainisha kuwa mkoa huo una zaidi ya kesi 80 za vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza kwa msisitizo, RC Sendiga alisema wanawake wanapaswa kuwa na hekima ya kutenganisha majukumu yao ya uongozi na majukumu ya kifamilia.

“Wakina Mama amkeni na mfahamu nafasi na thamani zenu. Mwanamke kufahamu haki yako hakumaanishi usimuheshimu mumeo. Tukisimama hapa sisi ni viongozi, lakini tukirudi nyumbani sisi ni wake na mama wa familia, lazima tujue kucheza na nafasi hizo mbili,” alisema.

Aidha, alionya tabia ya baadhi ya wanawake kujiona bora ndani ya nyumba hali inayochangia migogoro ya ndoa.

“Kuna wakati tunapata matatizo kwa sababu ya kujifanya tuna masharubu ndani. Ndani ya nyumba mwenye sharubu ni mmoja. Tunapodai haki zetu, basi na sisi tutimize wajibu wetu kama wake,” aliongeza.




RC Sendiga pia aliwakumbusha wanawake umuhimu wa malezi, usafi na mapenzi ndani ya familia, akisema kutokujali majukumu ya nyumbani kunasababisha migogoro na kuvuruga mahusiano.

“Akina Baba nao wana mioyo, wanahitaji kutunzwa. Ukisema huna muda wa kumtunza mume wala watoto, tutasaidiana vipi? Mahaba hayataki kelele, yanataka busara na upole,” alisema.



Kwa upande mwingine, aliwataka wanawake kuepuka tamaa ya fedha na miradi mingi isiyo na tija huku wakisahau majukumu ya msingi ya kifamilia, akisisitiza kuwa familia imara ni msingi wa jamii salama na taifa lenye maendeleo.

RC Sendiga alihitimisha kwa kutoa wito kwa viongozi wa jumuiya hiyo kuendelea kutoa elimu ya ndoa, malezi na maadili ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia na kujenga familia zenye mshikamano ndani ya Mkoa wa Manyara.

No comments:

Post a Comment