RUWASA YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MPANGO MKAKATI MIAKA MITANO IJAYO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 20, 2026

RUWASA YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MPANGO MKAKATI MIAKA MITANO IJAYO



Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imekutana na wadau wake wa ndani na nje ya nchi ikiwemo Wizara ya Maji na Benki ya Dunia katika kikao cha kujadili Mpangomkakati wa miaka mitano wa taasisi hiyo unaotoa mwelekeo wa vipaumbele vya kuimarisha huduma endelevu ya Maji safi ya bomba kwa wakazi wa maeneo ya vijijini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Februari 20, 2026, mwakilishi kutoka Wizara ya Maji Mha. Mashaka Sitta ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Uendeshaji na Matengenezo alisema mwelekeo wa RUWASA kuelekeza nguvu zaidi katika kuimarisha huduma endelevu ya maji ni jambo muhimu kwa sasa kwani tayari imeshajenga miradi mingi vijijini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa RUWASA Titus Mkapa ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Mha. Wolta Kirita aliwapongeza na kuwashukuru wadau wote wa maendeleo wanaoshirikiana na taasisi hiyo ambapo alisema baadhi ya vipaumbele katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kuhakikisha huduma ya maji vijijini inakuwa imara na endelevu pamoja na kuimarisha eneo la data na takwimu.

Akitoa maelezo ya awali, Mkurugenzi wa Mipango wa RUWASA Enock Wagala alisema kuwa, nyaraka hiyo ya Mpangomkakati wa miaka mitano imeshapitia hatua tofauti za maandalizi na sasa inawasilishwa kwa wadau wa maendeleo hususan wa maji vijijini ili watoe maoni na michango yao katika kuboresha na kuwa sehemu muhimu ya mpangomkakati huo wakati wa utekelezaji wake.

Mkurugenzi Wagala alitaja maeneo makuu Matano ambayo yamepewa kipaumbele zaidi katika Mpangomkakati huo kuwa ni pamoja na uendelevu wa huduma ya maji vijijini, kujenga miradi katika vijiji 1575 vilivyobaki, kuimarisha mbinu za upatikanaji wa fedha, kukamilisha ujenzi wa miradi 878, na kujenga na kuimarisha huduma za usafi wa mazingira vijijini.

Takribani taasisi za wadau 40 walihudhuria kikao hicho ambapo baadhi ya wadau hao ni Wizara ya Maji, Benki ya Dunia, AfDB, Oikos ETS, Water Mission Tanzania, Global Water Center, TAWASANET, Water for Pepople, Netherland Development Organization, UNICEF, CRDB, World Vision Tanzania, Benki ya Equity, NMB, Global Water Partnership Tanzania na DPG WASH Secretariet.








No comments:

Post a Comment