
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Wanafunzi 10 waliofadhiliwa na Serikali wameanza masomo ya Shahada ya Uzamili katika Sayansi Data (Data Science), Akili Unde (Artificial Intelligence) na Sayansi Shirikishi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+).
Aidha, wanafunzi wengine 10 wanatarajiwa kuanza masomo hayo katika Indian Institute of Technology Zanzibar, hatua inayoonesha dhamira ya Serikali kuwekeza zaidi katika taaluma za teknolojia za kisasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda, amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanzisha ufadhili huo maalum wa Uzamili kutokana na mahitaji ya taifa katika maeneo ya teknolojia, ubunifu na uchambuzi wa takwimu.
Amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, akibainisha kuwa vyuo vilivyochaguliwa vinatoa mafunzo kwa vitendo katika makampuni makubwa ya teknolojia, jambo linalowawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa moja kwa moja katika sekta hiyo.
“Vyuo tunavyopeleka wanafunzi wa Samia Scholarship AI/DS+ vinatoa fursa ya mafunzo kwa vitendo na vinaendelea kudahili wanafunzi wetu,” amesema Prof. Mkenda.
Amefafanua kuwa wanafunzi waliopata ufadhili wanatoka katika shule za Serikali na zisizo za Serikali. Kwa ngazi ya Uzamili, udahili unafanyika kupitia mfumo wa maombi, tofauti na ngazi ya Shahada ya Kwanza ambapo wanafunzi huchaguliwa kulingana na ufaulu wao wa juu.
Waziri Mkenda ametumia fursa hiyo kuwataka wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia mfuko wa Samia Scholarship, akisisitiza kuwa Serikali imeamua kwa makusudi kuongeza nguvu katika masomo ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati).
Amesema juhudi hizo zinaonekana kupitia ujenzi wa shule maalum za wasichana za sayansi katika kila mkoa, upendeleo wa mikopo kwa wanafunzi wa sayansi kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, pamoja na utoaji wa ufadhili kwa wanafunzi waliomaliza Kidato cha Sita.
Prof. Mkenda pia amewataka wanafunzi waliopata ufadhili ngazi ya Shahada ya Kwanza kuangalia majina yao kupitia tovuti ya Wizara, Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) na NM-AIST.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Maulilio Kipanyula, amesema mpango wa Samia Scholarship Extended (SSE DS/AI+) ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kujenga wataalamu wa ndani wenye ushindani wa kimataifa, huku ukitoa fursa ya kubadilishana uzoefu na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Prof. Amos Nungu, ameishukuru serikali kwa kuipa tume hiyo jukumu la kuratibu mpango huo, akisema muitikio wa wanafunzi umekuwa mkubwa,
"Tukiwa waratibu, tunaamini mwitikio utaongezeka zaidi katika awamu zijazo. Tunajivunia fursa hii na tunaona picha kubwa ya maeneo ya kimkakati ya kuwekeza ili kupata wataalamu wa aina inayohitajika nchini," alisema Prof. Nungu.







No comments:
Post a Comment