SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA KUITANGAZA TANZANITE NA MADINI YA VITO NCHINI QATAR - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 25, 2026

SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA KUITANGAZA TANZANITE NA MADINI YA VITO NCHINI QATAR




📍Doha, Qatar.


Katika utekelezaji wa ahadi ya kurejesha thamani na hadhi ya madini ya vito ya Tanzanite, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mkakati thabiti wa kutangaza madini ya Tanzanite nchini Qatar ili kuongeza wigo wa masoko yake na kuvutia uwekezaji na utalii.

Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Februari, 2026 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde alipotembelea Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar na kufanya mazungumzo na watumishi wa ubalozi.

"Soko la Tanzanite miaka ya hivi karibuni lilionekana kushuka kidogo na ndiyo maana hata bei imeshuka. Mhe. Rais ameskia kilio cha wachimbaji na wafanyabiashara wa Tanzanite na kutuagiza Wizara ya Madini kuhakikisha tunarudisha hadhi ya madini haya duniani kote ili yawe na manufaa kwa Taifa letu, " amesema Mhe. Mavunde.

Amesema Wizara inatekeleza kwa vitendo maelekezo hayo ya Mhe. Rais. kuhakikisha inaendelea kuyatangaza na kuyafikia masoko mbalimbali duniani na kuwaambia Tanzanite inatoka Tanzania na inapatikana kwa wingi.

Waziri Mavunde ameonesha kwamba mkakati huo wa Serikali ni muhimu na umekuja wakati muafaka kwani imeonekana baadhi ya nchi duniani kutokufahamu kama madini ya Tanzanite yanatoka Tanzania, hali ambayo inapelekea kuiondolea soko ambalo lingesaidia pia kutangaza utalii nchini.

Vilevile, Mhe. Mavunde amebainisha kuwa Tanzania imebarikiwa madini ya aina mbalimbali yakowemo ya vito, lakini Tanzanite ni ya kipekee na ni utambulisho wa Taifa kwani madini hayo hayapatikani popote duniani zaidi ya Tanzania, ni lazima kujivunia huku ikiyatangaza na kulinda sifa hiyo ya kipekee ambayo nchi imejaliwa kuwa na madini hayo.

Akishauri namna bora ya kuwafikia wadau wengi na kuwaeleza fursa za uwekezaji nchini Tanzania, Waziri Mavunde amekubaliana kuratibu kwa pamoja na Ofisi ya Ubalozi kuandaa ushiriki wa wafanyabiashara wa madini ya vito kutoka Tanzania kwenye maonesho ya madini yatakayofanyika Mwezi Aprili Doha-Qatar.

Awali, akimkaribisha Waziri nchini Qatar, Mhe Habibu Awesi Mohamed Balozi wa Tanzania nchini Qatar amemshukuru kwa kutembelea Qatar na kusisitiza kuwa zipo fursa nyingi kwa upande wa Sekta ya Madini ambazo zikifunguliwa zitaleta manufaa na tija kwa Taifa letu na kuchangia ukuaji wa uchumi.




No comments:

Post a Comment