SERIKALI YAIPONGEZA IAA KWA KUONGOZA MAGEUZI YA KIDIGITALI NA KUSUKUMA UTAFITI NA MAENDELEO KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2025–2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 6, 2026

SERIKALI YAIPONGEZA IAA KWA KUONGOZA MAGEUZI YA KIDIGITALI NA KUSUKUMA UTAFITI NA MAENDELEO KUELEKEA DIRA YA TAIFA 2025–2050


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (mwenye joho jekundu katikati), akiongoza Maandamano ya Kitaaluma katika Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha, ambapo alikuwa Mgeni Rasmi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli na Kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha, ambapo pamoja na mambo mengine aliwasihi wanafunzi na wahitimu wa Shahada ya Uzamili kutumia tafiti zao kutoa majibu ya changamoto halisi zinazolikabili Taifa kama vile usimamizi wa fedha za umma, ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira, ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akiwatunuku Wahitimu wa Shahada ya Uzamili 2,250 wa fani mbalimbali katika Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.

Baadhi ya wahitimu wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (hayupo pichani), wakati wa Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (hayupo pichani), wakati wa Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, akizungumza wakati wa wakati wa Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha, ambayo yamekuwa na jumla ya wahitimu 2,250 kati yao wanaume ni 1,369 sawa na asilimia 60.8 na wanawake 881 sawa na asilimia 39.2 ambao wametunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani kumi na tano (15).

Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb) (Katikati aliyeketi mwenye joho jekundu), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa Shahada ya Uzamili katika fani kumi na tano (15), yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha, ambayo yamekuwa na jumla ya wahitimu 2,250 kati yao wanaume ni 1,369 sawa na asilimia 60.8 na wanawake 881 sawa na asilimia 39.2.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha)


Na. Joseph Mahumi, WF, Arusha


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar(Mb), amekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kufanya mageuzi ya kidigitali, ufanyaji wa tafiti, maendeleo pamoja na mipango na mikakati ya kuboresha na kuongeza ufanisi kwenye utoaji wa mafunzo, na ushauri wa kitaalam, ambazo ni miongoni mwa vichocheo vya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025-2050.

Hayo yasemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya Chuo hicho, yaliyofanyika katika Hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.

Mhe. Luswetula alisema kuwa mchango wa IAA katika uchumi wa Taifa ni mkubwa kwa kuwa kimeendelea kuzalisha wataalam wa fedha, uhasibu, uchumi, kodi, utalii, usimamizi biashara, benki, ununuzi na ugavi, masoko, bima, TEHAMA na nyingine nyingi.

Alisema kuwa Wataalam hao wamekuwa mhimili muhimu katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, usimamizi wa fedha za umma, sekta binafsi, taasisi za kifedha na miradi ya maendeleo.

Aliongeza kuwa Kupitia wahitimu wake, Chuo kimechangia kwa vitendo katika kukuza uwajibikaji, uwazi na nidhamu ya kifedha nchini.

“Niwapongeze IAA mmeendelea kudhihirisha umahiri mkubwa katika kuandaa rasilimali watu mahiri, wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa Taifa letu” alisema Mhe. Luswetula.

Aidha, Mhe. Luswetula alikisifu Chuo cha IAA kwa kuwa kinara katika kuboresha mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa sambamba na kuimarisha tafiti na ushauri wa kitaalam.

“Mageuzi ya kidigitali ni kichocheo muhimu cha maendeleo hususan katika kuboresha ukuaji wa uchumi na kuimarisha huduma za jamii ikiwemo elimu. Serikali inatambua na kupongeza juhudi za IAA katika kuwekeza kwenye mifumo ya kidigitali na katika kuimarisha ufanisi wa utoaji wa elimu kwa njia bunifu,” aliongeza Mhe. Luswetula.

Mhe. Luswetula alitumia fursa hiyo pia kuwasihi wanafunzi na wahitimu wa Shahada ya Uzamili kutumia tafiti zao kutoa majibu ya changamoto halisi zinazolikabili Taifa kama vile usimamizi wa fedha za umma, ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira, ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia.

“Tafiti zenu ziwe chachu ya sera bora, maamuzi sahihi na maendeleo endelevu kwa wananchi na Taifa letu,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo jumuishi yanayomgusa kila Mtanzania, huku sekta za fedha, uhasibu, uchumi, benki, usimamizi wa biashara na miradi zikiwa nguzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za Taifa zinakusanywa, zinapangwa, zinatumika na zinadhibitiwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Aidha, alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha, itaendelea kuhimiza na kuunga mkono Vyuo vya Elimu ya Juu vinavyoendana na dira ya Taifa ya kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa na ujuzi.

“Wizara itaendelea kushirikiana na vyuo hivi katika kuweka mazingira wezeshi ya kifedha na kisera yatakayowezesha kuimarishwa kwa kozi za kimkakati, tafiti zenye tija, na maandalizi ya wataalam wanaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.” Alisema Mhe. Luswetula

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, alisema kuwa Chuo hicho kimejipanga kuendelea kutoa wahitimu mahiri kwa kuwekeza katika rasilimali watu, hususani wahadhiri wenye sifa, uzoefu wa kitaaluma na kitaalam, pamoja na kuimarisha mbinu shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji.

Alisema kuwa IAA imejipambanua kama Taasisi inayozalisha wahitimu mahiri, wabunifu, na wenye uwezo wa kuchambua na kutatua changamoto za jamii inayowazunguka, maeneo wanayofanyia kazi zao na Taifa kwa ujumla.

Wahitimu wa Shahada ya Uzamili wa IAA wanatambulika kwa ubora wa taaluma, maadili, na weledi wa kitaaluma katika sekta mbalimbali.

“Ubora huu unatokana na mitaala inayozingatia mahitaji ya sasa ya soko la ajira, maendeleo ya teknolojia, na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii. IAA imeendelea kuhakikisha kuwa programu zake za Uzamili zinawajengea wanafunzi ujuzi wa kina, fikra pevu, na uwezo wa uongozi” alisema Dkt. Tulli.

Aliongeza kuwa Baraza la Uongozi wa Chuo litaendelea kusimamia kwa karibu mipango na kimkakati ya Chuo, ili kuhakikisha IAA inaendelea kuwa Taasisi kinara katika elimu ya juu, tafiti, na ushauri wa kitaalamu nchini na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, alisema kuwa kwa kutambua mabadiliko ya kasi katika mahitaji ya soko la ajira na uongozi wa kitaifa, Chuo hicho kinaendelea kuimarisha huduma za ufundishaji na ujifunzaji kwa kuboresha mitaala, mbinu za kufundishia, na mifumo ya tathmini ili kuendana na sera, mikakati, na dira ya maendeleo ya Taifa 2025-2050.

Alisema kuwa IAA imeweka mkakati mahususi wa kuwawezesha wahadhiri wengi zaidi kusomea Shahada ya Uzamivu ndani na nje ya nchi, ili kukidhi ongezeko la idadi ya wanafunzi wa Uzamili linaloendelea kushuhudiwa kila mwaka ambapo katika mwaka wa masomo 2025/2026 jumla ya wahadhiri 115 wamepelekwa kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

“Mkakati huu unalenga kuhakikisha uwiano sahihi kati ya wanafunzi na wahadhiri, kuimarisha usimamizi wa tafiti, na kuongeza uwezo wa Chuo katika uzalishaji wa wataalam wanaokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa” alisema Prof. Sedoyeka.

Mahafali ya 27 (Duru ya Pili) ya IAA, imewahusisha jumla ya wahitimu 2,250 kati yao wanaume wakiwa 1,369 sawa na asilimia 60.8 na wanawake 881 sawa na asilimia 39.2 ambao wametunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani kumi na tano (15) .

Fani hizo ni (Accountancy), Uhasibu na Fedha (Accounting and Finance), Fedha na Benki (Finance and Banking), Fedha na Uwekezaji (Finance and Investment), Usimamizi wa Miradi (Project Planning Management), Usimamizi wa Taarifa (Information Management), Uchumi na Fedha (Economics and Finance), Usimamizi wa Elimu (Education Management), Usimamizi wa Rasilimali watu (Human Resource Management) na Amani na Usalama (Peace and Security ). Fani nyingine ni Usimamizi wa Biashara (Master of Business Administration in Corporate Management), Usimamizi wa Biashara katika Teknolojia ya Habari (MBA-Information Technology), Usimamizi wa Biashara katika Uandaaji na Utekelezaji wa Sera (MBA-Policy Development and Execution), Usimamizi wa Biashara katika Uongozi (MBA-Leadership and Governance), Usimamizi wa Biashara katika Ununuzi na Ugavi (MBA-Procurement and Supply Chain Management).

No comments:

Post a Comment