SERIKALI YASUKUMA UWEKEZAJI MKULAZI, MBUNGE MVOMERO ASISITIZA MABORESHO YA BARABARA NA SOKO LA MIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 25, 2026

SERIKALI YASUKUMA UWEKEZAJI MKULAZI, MBUNGE MVOMERO ASISITIZA MABORESHO YA BARABARA NA SOKO LA MIWA


Mapema leo Februari 26, Mbunge wa Jimbo la Mvomero Sara Msafiri Ally ameongozana na Waziri wa Kilimo Daniel Chongolo pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo, katika ziara ya kutembelea Kiwanda cha Sukari Mkulazi kilichopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Akiwa katika ziara hiyo ya kukagua miradi ya uwekezaji uliofanywa na Serikali, Mheshimiwa Sara Msafiri Ally amemuomba Waziri wa Uwekezaji kuangalia kwa kina sekta ya barabara ndani ya Jimbo la Mvomero, hususan katika maeneo yenye uwekezaji mkubwa.

 Amesisitiza kuwa maboresho ya miundombinu ya barabara yatawawezesha wawekezaji na wakulima kunufaika zaidi na shughuli za uzalishaji na masoko.

Mbunge huyo pia ameibua changamoto ya wakulima wa miwa, akieleza kuwa kiwango kikubwa cha miwa kinachomwa mashambani kutokana na kukosa soko la uhakika, hali inayotokana na kiwanda kuzidiwa uwezo wa kuchakata.

 Amesema hali hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa wakulima wengi, na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Uwekezaji kutafuta suluhisho la kudumu ili kuimarisha soko la miwa na kulinda kipato cha wakulima.

Kwa upande wake, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali inaendelea kutekeleza ajenda ya kusukuma uwekezaji katika mashirika ya umma ili kuongeza tija na uzalishaji.

Ameeleza kuwa Kiwanda cha Sukari Mkulazi kimepiga hatua muhimu, hususan kwa kuwa na uwezo wa kuzalisha sukari ya matumizi ya viwandani, jambo linalochangia kupunguza utegemezi wa sukari kutoka nje ya nchi.

Aidha, amewahimiza wadau kupanua wigo wa masoko ya sukari hiyo ili kuhakikisha nchi inafikia lengo la kujitegemea kwa asilimia 100 katika uzalishaji wa sukari, sambamba na kulinda maslahi ya wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

Naye Waziri wa Wa Kilimo Daniel Chongolo ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na sekta ya Mipango na uwekezaji ili kuhakikisha miradi ya uwekezaji inaenda kuimarika na kuleta manufaa kwa taifa

No comments:

Post a Comment