SERIKALI YAZITAKA TAASISI KUTEKELEZA AGIZO LA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 4, 2026

SERIKALI YAZITAKA TAASISI KUTEKELEZA AGIZO LA NISHATI SAFI YA KUPIKIA




Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


SERIKALI imezitaka taasisi zote zinazolisha watu zaidi ya 100 nchini kuhakikisha zinaendelea kutekeleza agizo la kutumia nishati safi ya kupikia, ili kulinda mazingira na afya za wapishi kwa kuondokana na madhara ya moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyo salama .

Mhe. Makamba amesema kuwa kati ya taasisi zipatazo 30,000 zilizopo nchini, ni taasisi 1,136 pekee ndizo zinazotumia nishati safi ya kupikia, hali inayoonesha bado kuna kazi kubwa ya kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo muhimu kwa ustawi wa jamii.

Wito huo umetolewa leo Februari 4, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, wakati akizindua Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana.

Amesema changamoto kubwa si upatikanaji wa nishati safi, bali ni ukosefu wa elimu ya matumizi sahihi ya nishati hiyo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi zake na jamii kwa ujumla.

“Leo tumeweka alama ya kudumu katika kuhifadhi mazingira na kulinda afya zetu kwa kuzindua mradi huu wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana,” amesema Mhe. Makamba.

Mradi huo umetekelezwa chini ya Wizara ya Nishati na umegharimu takribani Shilingi milioni 30, ukiwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhamasisha taasisi nyengine zinazohudumia watu wengi kuachana na matumizi ya nishati isiyo salama na kutumia nishati safi, ikiwemo gesi ya kupikia (LPG).

Naibu Waziri ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.6 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 23.2 mwaka 2026, huku zaidi ya taasisi 1,000 zikiwa tayari zimehamia katika matumizi ya nishati safi, ikiwemo shule hiyo ya Bunge Wasichana.

Katika uzinduzi huo, Mhe. Makamba pia amezindua Klabu ya Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking Club), akieleza kuwa ni klabu ya kwanza kuanzishwa nchini Tanzania, na kuwataka wanafunzi kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi katika jamii zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweru, amesema Shule ya Sekondari Bunge Wasichana ni miongoni mwa shule vinara wilayani humo na kuipongeza Serikali kwa kuifanya shule hiyo kuwa kipaumbele cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Mhe. Jonas Mbunda, amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wote, huku Kamati ikiridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati nchini.

Akitoa taarifa ya mradi, Naibu Katibu Mkuu Nishati, James Mataragio, amesema tafiti zinaonesha zaidi ya watu milioni mbili hufariki kila mwaka duniani kutokana na athari za matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia, huku nchini Tanzania athari hizo kubwa zaidi zikiwa kwa wanawake na watoto.

Amesema uzinduzi wa mradi huo ni utekelezaji wa sera ya taifa inayolenga kuondokana na matumizi ya nishati isiyo salama na kujikita katika matumizi ya nishati safi, hatua itakayosaidia kulinda mazingira, kuboresha afya na kuongeza tija hata katika ufaulu wa wanafunzi.

Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bunge Wasichana, Richard Msana alisema shule hiyo yenye wanafunzi 555 imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za nishati ya kupikia baada ya kuachana na matumizi ya kuni na kuhamia katika gesi.

Amesema kuanzia Julai 2020 hadi Mei 2022, shule ilikuwa ikitumia takribani shilingi milioni 10.5 kwa kila miezi mitatu kununua kuni. Baadaye walipoanza kutumia mkaa mbadala, gharama zilishuka hadi kufikia shilingi milioni 2.7 na hivi sasa, kupitia mradi wa matumizi ya gesi, shule imenunua tani moja ya gesi iliyotumika kwa miezi miwili, ambapo matumizi ni wastani wa shilingi milioni 1.3 kwa mwezi, kiwango ambacho ni nafuu zaidi kiuchumi.




No comments:

Post a Comment