
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, KONDOA
Serikali imetenga shilingi bilioni 25.8 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka nishati safi ya kupikia katika taasisi 453 zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku, ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Taifa ya kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Akizindua awamu ya kwanza ya mradi huo Februari 17, 2026 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa mkoani Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema mradi huo unahusisha shule 52 za sekondari pamoja na chuo kimoja cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
Mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa asilimia 100 wa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na unahusisha usimikaji wa mifumo ya gesi ya LPG, ufungaji wa majiko banifu pamoja na usambazaji wa mkaa mbadala.

Makamba amesema katika awamu ya kwanza, taasisi 53 zitanufaika, huku awamu ya pili ikihusisha taasisi 400 katika mikoa yote nchini, hatua inayolenga kuhakikisha taasisi zote zinazohudumia zaidi ya watu 100 zinatumia nishati safi ya kupikia.
Ameeleza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha taasisi hizo zinaachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida kwa kulinda afya za wananchi na mazingira.

“Ili mradi huu uwe endelevu, nitoe wito kwa Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na TAMISEMI kusimamia mifumo iliyofungwa ili iwe endelevu na ihamasishwe kuigwa na jamii,” amesema Makamba.
Aidha, ameitaka sekta binafsi kuchangamkia fursa za uzalishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Jonas Mbunda, amempongeza Rais kwa kuanzisha na kugharamia mpango huo, akisema utalinda afya na mazingira.
Naye Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay, amesema mradi huo utapunguza matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi za elimu, kuboresha afya na usalama wa wapishi na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa shule.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema takwimu zinaonesha matumizi ya nishati isiyo safi yamechangia uharibifu wa takribani hekta 46,606 za misitu kila mwaka, huku zaidi ya watu 33,000 wakifariki kutokana na athari za moshi wa kupikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, amesema mradi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa umegharimu shilingi milioni 54, ambapo limefungwa tanki la gesi lenye ujazo wa tani moja pamoja na mfumo wa mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya miwa.
Mkuu wa shule hiyo, Mwl. Flora Nusu, amesema mradi huo utapunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 40 na kuondoa athari za kiafya kwa wapishi na wanafunzi.






No comments:
Post a Comment