WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amewaagiza baadhi ya mawaziri alioambatana nao wabakie mkoani Tanga ili kufuatilia masuala yaliyoibuliwa na wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Masuala hayo yalitokana na hoja zilizoibuliwa kwenye mikutano ya hadhara na wabunge wa mkoa wa Tanga na wananchi mbalimbali kwenye sekta za ardhi, mifugo, kilimo, maji, elimu na barabara.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Februari 17, 2026) wakati akizungumza na wakazi wa Soni, Bumbuli katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye stendi ya Soni, wilayani Lushoto, mkoani Tanga.
Mapema, akijibu hoja kuhusu ubovu wa barabara wilayani Lushoto, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali cha kuanza ujenzi wa pande mbili wa barabara ya Soni - Bumbuli- Dindira hadi Old Korogwe.
“Barabara hii ilishatangazwa na sasa tunakamilisha taratibu za wakandarasi. Zikiwa tayari, mmoja ataanzia Soni kwa kujenga kilometa 22 na mwingine ataanzia Old Korogwe (KwaMeta hadi KwaShemsi) kwa kujenga kilometa 9.5,” alisema.
Alisema barabara ya sasa ya kutoka Mombo - Soni hadi Lushoto yenye urefu wa km. 32 imeshafanyiwa usanifu na inatafutiwa fedha ili iweze kufanyiwa upanuzi.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Msajili wa Hazina anamalizia uhakiki wa madeni ya zamani ya wakulima wa chai waliokuwa wanadai malipo katika kiwanda cha chai cha Mponde na kuongeza kuwa katika kipindi cha hivi karibuni hakuna madeni yoyote yaliyolimbikizwa.
Alisema kiwanda hicho ambacho kinahudumia Halmashauri mbili za Bumbuli na Korogwe, kinafanyiwa mpango wa kupata line nyingine ya uzalishaji ili kupunguza mlundikano wa majani ya chai yaliyovunwa. Alisema Bodi ya Chai imeshanunua kiwanda kingine huko Korogwe ambacho kinatarajiwa kuanza kazi kabla ya Juni, mwaka huu ili kisaidie kupunguza mzigo unaoenda kiwanda cha Mponde.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua na kuzindua shule mpya ya sekondari ya amali ya Majulai iliyopo katika kijiji cha Majulai, Kata ya Mwangoi, Tarafa ya Mlalo wilayani Lushoto.
Shule hiyo ambayo imejengwa kwa kupitia mradi wa SEQUIP na tayari imesajiliwa, ina walimu sita na wanafunzi 89 ambao walianza masomo Januari 13, 2026..
Akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Mkuu wa shule ya Sekondari Shita ambayo ni shule mama, Mwalimu Ramadhani Mohammed alisema mradi huo ambao umegharimu sh. milioni 584.28 ulianza kutekelezwa Oktoba 23, 2024 na hadi sasa umetumia sh. milioni 581.81 na kwamba sh. milioni 2.46 zilizobakia ni za angalizo, kukamilisha ujenzi wa tenki na kulipa mafundi.



No comments:
Post a Comment