
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akipokea kitabu kinachohusu ushirikiano na nchi za Afrika kutoka kwa Balozi wa India nchini Mhe. Bishwadip Dey, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiteta jambo na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Bishwadip Dey, baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao kuhusu ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akieleza kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na India, wakati wa mkutano kati yake na Balozi wa India nchini Mhe. Bishwadip Dey, uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.

Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Bishwadip Dey, akieleza kuhusu uanzishwaji wa viwanda nchini ili kukuza ushirikiano wakati wa mkutano na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa nne kushoto), akiongoza mkutano kati yake na Balozi wa India nchini Mhe. Bishwadip Dey (wa pili kulia), kuhusu ushirikiano kati ya pande hizo mbili, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Ujumbe wa India ukiongozwa na Balozi wa India nchini Tanzania Mhe. Bishwadip Dey (katikati), wakiwa katika Mkutano na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)
Na Peter Haule na Josephine Majura, WF, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania na India zimekubaliana kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini, Mhe. Bishwadip Dey, aliyefika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha. jijini Dar es Salaam kujitambulisha.
Mhe. Balozi Omar alisema kuwa katika kipindi ambacho Tanzania inatekeleza Dira ya Taifa 2050, kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Serikali ya India, wakati ambapo uhusiano wa kidiplomasia, kijamii na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kuimarika.
Alieleza kuwa uhusiano wa Tanzania na India ni wa kihistoria na umejengwa katika misingi imara ya ushirikiano wa muda mrefu, uliowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta za maji na afya, yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
“Uhusiano wetu ni wa muda mrefu na umeanza hata kabla ya kuanzishwa rasmi kwa uhusiano wa kidiplomasia ambapo watu kutoka pande hizi mbili walikuwa wakisafiri na kufanya biashara kupitia Bahari ya Hindi, na leo hii ushirikiano wetu umejikita katika nyanja za kibalozi, kiuchumi na kijamii,” alisema Balozi Omar.
Akizungumzia sekta ya maji, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia ushirikiano na India, huku changamoto zilizojitokeza zikishughulikiwa kwa kushauriana na kushirikiana kwa karibu kati ya nchi hizo mbili.
Katika sekta ya elimu, Mhe. Balozi Omar alibainisha kuwa India imeanzisha chuo Zanzibar kinachotoa mafunzo ya Sayansi ya Data na Akili Unde (AI), pamoja na kozi za muda mfupi na mrefu.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo si tu inanufaisha Watanzania, bali pia wanafunzi kutoka mataifa mengine ya Afrika, hivyo kutoa fursa muhimu ya kukuza ujuzi na teknolojia barani humo.
Aidha, alieleza kuwa India imeendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania, hususan katika sekta ya afya, ambapo wataalamu wengi wamepata mafunzo nchini humo ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya.
Kwa upande wake, Balozi wa India nchini, Mhe. Bishwadip Dey, alisema kuwa thamani ya biashara kati ya India na Tanzania imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka ya karibuni.
Alisema kuwa katika mwaka 2020/2021, biashara kati ya nchi hizo mbili ilikuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 2.3, huku ikifikia dola bilioni 8.6 mwaka 2024/2025.
Alibainisha kuwa miongoni mwa bidhaa zinazouzwa kutoka India kwenda Tanzania ni mashine na kemikali, huku akisisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuhamasisha uwekezaji wa moja kwa moja katika viwanda, ikiwemo vya vifaa tiba na vyombo vya usafiri, badala ya kuishia kwenye usafirishaji wa bidhaa pekee.
Mhe. Balozi Dey aliongeza kuwa tayari kuna wawekezaji kutoka India waliowekeza katika sekta ya kilimo, viwanda vya kuzalisha nondo, pamoja na maeneo mengine ya uzalishaji yanayochangia ajira na kukuza uchumi.
Alisema ziara yake ilikuwa ni kwa ajili ya kujitambulisha na amewasilisha kitabu kinachoelezea historia na mafanikio ya ushirikiano kati ya India na nchi za Afrika.

No comments:
Post a Comment