
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) tarehe 9 Februari, 2026, limepongezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bw. John Tilubuzya, kwa kuendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wanaotumia usafiri majini. Kupitia elimu hiyo itaongeza uelewa kuhusu kanuni, sheria na matumizi salama ya vyombo vya usafiri majini.
Bw. Tilubuzya ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa TASAC walipotembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kupata ridhaa ya kutoa elimu kwa wadau mbalimbali katika mialo iliyopo Mkoa wa Mtwara.

“Nawakaribisha kwa dhati katika Mkoa wa Mtwara na nawapongeza sana kwa juhudi zenu za kuendelea kuelimisha umma kuhusu usafiri majini. Kazi mnayoifanya ni muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri majini pamoja na kuwalinda watumiaji wake, na ina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama na uelewa kwa wananchi,” amesema Bw. Tilubuzya.
Aidha, Bw. Tilubuzya ameahidi kuwepo kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na TASAC katika kufanikisha majukumu ya kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na watumiaji wake. Amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana na TASAC katika shughuli mbalimbali za uelimishaji kwa umma na usimamizi ili kuongeza uelewa wa masuala ya usalama kwa wadau wote.
Hata hivyo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoani Mtwara Bw. Joseph Myaka amewaasa wamiliki, wavuvi na wadau mbalimbali wa usafiri majini kuzingatia sheria na kanuni kwa kubeba abiria kwa idadi inayolingana na uwezo wa chombo kutokana na leseni iliyotolewa ili kupunguza ajali.
“Chombo cha abiria kibaki kuwa cha abiria na chombo cha mizigo kibaki kuwa cha mizigo ili kuepuka kubeba abiria na mizigo kwenye chombo kimoja, pia kuhakikisha wakati wote wanavaa jaketi okozi “life jacket” wawapo katika vyombo vya usafiri majini ili kupunguza ajali za usafiri majini, amesema Myaka”.
Wadau walioshiriki wamepongeza juhudi za TASAC kwa kuendelea kuwafikia moja kwa moja katika maeneo yao ya kazi na kutoa elimu yenye tija. Wamesema elimu hiyo itasaidia kupunguza ajali za majini na kuongeza usalama wa vyombo na watumiaji wake, huku wakiahidi kushirikiana na TASAC katika kutekeleza miongozo ya usalama kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Hakika tunaishukuru TASAC kwa kutufikia na kutupatia elimu hii muhimu ya usalama wa usafiri majini. Tunaomba iendelee kutolewa mara kwa mara, hususan hapa Mtwara na pia katika maeneo mengine, ili kuongeza uelewa wa jamii kuhusu shughuli zinazofanywa na TASAC na kuendelea kuimarisha usalama wa majini kwa manufaa ya watumiaji wote ili kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika.” Amesema Yusufu Chunda.
Elimu kuhusu Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira Majini imefanyika katika fukwe za Msimbati, Kirambo na Msemo ilianza rasmi tarehe 9 na itahitimishwa tarehe 13 Februari, 2026







No comments:
Post a Comment