
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amekagua na kuridhishwa na maendeleo ya matengenezo ya barabara ya Dodoma–Iringa katika eneo la Fufu, ambalo lilikuwa likikumbwa na changamoto ya kujaa maji wakati wa mvua na kusababisha adha kwa wananchi na wasafiri.

Waziri Ulega amefanya ukaguzi huo leo, Februari 25, 2026, akiwa njiani kuelekea mkoani Iringa kwa ziara ya kikazi. Akiwa eneo hilo, amempongeza Meneja wa TANROADS mkoani Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, kwa kusimamia na kukamilisha matengenezo ya sehemu hiyo pamoja na uwekaji wa taa 46 za barabarani ili kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Aidha, Waziri Ulega amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga, kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa makalavati katika eneo la Manzase pamoja na kuinua tuta la barabara ili kuondoa tatizo la maji kujaa, hususan kipindi cha mvua.
Hatua hiyo inalenga kuboresha miundombinu ya barabara na kuhakikisha usafiri unakuwa wa uhakika katika msimu wote wa mwaka, sambamba na kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.






No comments:
Post a Comment