
Na Hadija Bagasha - Tanga
Imeelezwa kuwa ongezeko la mifarakano na kuvunjika kwa ndoa nyingi kwenye jamii imekuwa chanzo kikuu cha mmomonyoko wa maadili kwa watoto wengi na kwamba changamoto za kifamilia zimekuwa zikiathiri kwa kiasi kikubwa makuzi ya watoto na kuwaingiza katika hatari ya kuharibika kitabia na hata kuathirika kisaikolojia.
Kauli hiyo imetolewa na Mchungaji Ibrahim Joram wakati wa mahafali ya nne ya Chuo cha Theolojia na uongozi cha Eclea Kampasi ya Tanga, ambapo alisisitiza kuwa athari za kuvunjika kwa ndoa haziishii kwenye mgawanyiko wa mali au makazi, bali huacha alama ya kudumu katika nafsi za watoto.

Kwa mujibu wa mchungaji huyo, watoto wanaokulia katika mazingira yenye migogoro ya mara kwa mara au wazazi waliotengana hukosa msingi imara wa malezi na mwongozo wa karibu kutoka kwa pande zote mbili za wazazi ambapo hali hiyo huwafanya baadhi yao kukosa upendo, uangalizi na haki ya msingi ya kusikilizwa na kueleweka, jambo linaloweza kuwafanya watafute faraja au uthibitisho nje ya familia, wakati mwingine kujiingiza katika makundi au matendo yasiyofaa.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa huduma ya Eclea Tanzania Reverine Mdimi, alieleza kuwa watoto wengi baada ya wazazi kutengana hujikuta wakikumbwa na msongo wa mawazo, hasira, huzuni au kukosa mwelekeo sahihi wa maisha hivyo bila msaada wa karibu wa wazazi, walezi au jamii, watoto hao huweza kujiingiza katika mienendo mibaya inayoweza kuharibu mustakabali wa maisha yao.
Wakizungumza katika mahafali hayo, wachungaji waliwataka wazazi kujijenga kiimani na kiroho ili kuimarisha misingi ya ndoa na familia na kwamba imani thabiti humsaidia mzazi kuwa na uvumilivu, busara na uwezo wa kusuluhisha migogoro kwa njia ya mazungumzo badala ya kuishia katika kuvunjika kwa ndoa.
Naye mchungaji Joas Stephano wa makanisa ya pentecoste motomoto aliwahimiza wanandoa kutafuta ushauri wa kitaalamu na wa kiroho mapema wanapokumbana na changamoto, ili kulinda ustawi wa watoto wao.
Kwa upande wa taasisi za elimu ya dini, wachungaji hao walibainisha kuwa mafunzo yanayotolewa katika Chuo cha Eclea hayalengi tu masomo ya kitheolojia, bali pia yanatoa elimu ya maisha.
"Eclea inatoa masomo rasmi yanayohusika na mambo kama hayo moja msamaha na maridhiano, mbili ndoa na malezi bora ni mafunzo tunayoyatoa kwa kina zaidi pamoja na kutoa ushauri wa kijinsia kwa maana tunawashauri watu namna gani bora ya kutatua migogoro ya kifamilia hasa kwenye eneo hili la ndoa na familia, "akisisitiza Mchungaji Mdimi.
Walieleza kuwa viongozi wa dini wanaohitimu masomo ya kidini wanatarajiwa kuwa mwanga katika jamii, wakifundisha si tu neno la Mungu, bali pia misingi ya malezi bora, maadili na utatuzi wa migogoro ya kifamilia.
Mahafali hayo yalikuwa fursa ya kuwakumbusha wahitimu kuwa huduma yao kwa jamii inapaswa kuanzia katika kuimarisha familia, ambayo ndiyo msingi wa taifa lolote huku Wachungaji wakiwahimiza wahitimu kuwa mabalozi wa amani na maridhiano, wakisaidia kurejesha matumaini kwa familia zinazokumbwa na misukosuko na kulinda kizazi dhidi ya athari za kuvunjika kwa ndoa.
Kuvunjika kwa ndoa ni changamoto inayoweza kuzuilika endapo wazazi watachukua hatua za makusudi kujenga upendo, mawasiliano na imani ndani ya familia. Ni wito kwa jamii nzima kusimama pamoja kulinda maadili ya watoto, kwani mustakabali wa taifa huanzia katika uimara wa familia.












No comments:
Post a Comment