Wanawake wanaojihusisha na uvuvi wa kiwango kidogo wamepewa mafunzo maalum ya haki za binadamu yanayolenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali za maji na maamuzi muhimu yanayohusu sekta ya uvuvi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanaendeshwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Denmark ya Haki za Binadamu (DIHR), yakihusisha viongozi wa Chama cha Wanawake Wavuvi Tanzania (TAWFA) kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bwn.Patience Ntwina, amesema mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa haki za binadamu kwa wanawake wavuvi ili waweze kuwa walinzi na watetezi wa haki zao pamoja na za wengine katika sekta ya uvuvi.
Amesema wanawake wavuvi wadogo ni mhimili muhimu wa usalama wa chakula, ajira na kukuza uchumi wa taifa, hivyo ni lazima wawe na uelewa wa haki zao na nafasi yao katika maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, Margrethe Dominic, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uvuvi, akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema sekta ya uvuvi nchini inategemea kwa kiasi kikubwa wavuvi wadogo wanaofikia asilimia 90, huku wanawake wakichangia pakubwa katika kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi.
Ameeleza kuwa licha ya mchango wao mkubwa, wanawake bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kushiriki katika maamuzi, ukosefu wa fursa sawa na unyanyasaji wa kijinsia, hali inayohitaji juhudi za pamoja kuikabili.
Akitoa salamu za Mwenyekiti wa TAWFA Taifa, Bi. Beatrice Mmbaga, viongozi wa chama hicho wameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na CHRAGG kwa kuendelea kuwashika mkono wanawake wavuvi, wakieleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uelewa na ujasiri wa kudai haki zao.
Wamesema kupitia mafunzo hayo, viongozi waliopata nafasi hiyo watakuwa mabalozi wa elimu kwa wanawake wengine ambao hawakushiriki, ili kuhakikisha haki na ushiriki wa wanawake katika sekta ya uvuvi unaimarishwa kote nchini.
Naye Katibu wa TAWFA Taifa, Hadija Malibiche, amesema bado mila kandamizi ni changamoto kubwa kwa wanawake wavuvi, hivyo kuna haja ya serikali na wadau kuendelea kuwekeza katika mafunzo na mifumo itakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu sekta ya uvuvi.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu ya kimkakati katika kuhakikisha wanawake wavuvi wanatambua, wanadai na wanalinda haki zao kwa maendeleo endelevu ya sekta ya uvuvi nchini.








No comments:
Post a Comment