WATUMISHI WA UMMA, WANANCHI WAPEWA NYENZO YA KUWASILIANA NA SERIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, February 16, 2026

WATUMISHI WA UMMA, WANANCHI WAPEWA NYENZO YA KUWASILIANA NA SERIKALI


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi (kushoto) akifuatilia wasilisho la mada kuhusu Mfumo wa e-Mrejesho wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa ofisi hiyo ambayo hutolewa kila siku ya Jumatatu kwenye ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Janet Mishinga akifafanua jambo alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Mfumo wa e-Mrejesho wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.

Wakurugenzi wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakifuatilia wasilisho la mada kuhusu Mfumo wa e-Mrejesho wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa ofisi hiyo yaliyofanyika katika ofisi hiyo jijini Dodoma.

Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakifuatilia wasilisho la mada kuhusu Mfumo wa e-Mrejesho wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa ofisi hiyo ambayo hufanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma. Wengine ni Watumishi wa ofisi hiyo.


Na. Veronica Mwafisi- Dodoma.


Serikali imewahimiza Watumishi wa Umma na wananchi kutumia Mfumo wa Kielektroni wa Kutuma, Kupokea na Kufuatilia Malalamiko, Mapendekezo, Maulizo na Pongezi Serikalini (e-Mrejesho) ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Maadili, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Janet Mishinga wakati akiwasilisha mada kuhusu mfumo huo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo jijini Dodoma.

Bi. Mishinga amesema mfumo wa e-Mrejesho ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Utawala Bora inayolenga kulinda maslahi ya wananchi wengi, kuhakikisha uwazi, kupiga vita rushwa, kuleta haki na usawa pamoja na kuhimiza uwajibikaji katika taasisi za umma.

Amesema kupitia Idara ya Usimamizi wa Maadili, ofisi hiyo imeendelea kusimamia utekelezaji wa mfumo huo ili kuhakikisha malalamiko na maoni ya wananchi yanapokelewa na kushughulikiwa kwa wakati, kwa lengo la kuboresha huduma za Serikali.

Aidha, amefafanua kuwa ufuatiliaji wa utekelezaji wa e-Mrejesho unasaidia kubaini mafanikio na changamoto zilizopo, pamoja na kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi katika kuwahudumia wananchi.

Kwa mujibu wa Bi. Mishinga, mfumo huo pia unaongeza ushirikishwaji wa watumishi wa umma na wananchi katika kuboresha utendaji wa Serikali kwa kutoa fursa ya maoni na mrejesho kwa njia ya kielektroni.


Serikali imeendelea kusisitiza matumizi ya teknolojia za kidijitali kama nyenzo muhimu ya kuimarisha utawala bora na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma.

No comments:

Post a Comment