Na Saidi Saidi – WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kudumisha upendo, umoja na mshikamano ili kujenga mazingira bora ya kazi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati wa sherehe ya watumishi wa Wizara hiyo (Maendeleo ya Jamii Day Gala 2026), iliyofanyika tarehe 6 Februari, 2026, katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Gwajima amesema kuwa mshikamano na upendo miongoni mwa watumishi ni msingi muhimu unaochangia mafanikio ya Wizara katika kuwahudumia wananchi, hususan makundi maalum yanayohitaji uangalizi wa karibu wa Serikali.
“Ni muhimu watumishi wakaishi kama familia moja, mheshimiane, mshirikiane na kusaidiana, kwani hilo ndilo litakalowezesha Wizara yetu kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema kuwa matukio kama Maendeleo ya Jamii Day Gala 2026 ni muhimu katika kujenga mshikamano na kuongeza morali ya watumishi kazini. Amesisitiza kuwa Wizara ina majukumu mazito ya kuwahudumia wananchi, hivyo ni lazima watumishi wake wawe na mahusiano mazuri, mshikamano na moyo wa kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha malengo ya Serikali.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Felister Mdemu, amesema uongozi wa Wizara utaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha watumishi kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kushirikiana. Ameongeza kuwa mshikamano, mawasiliano mazuri na kuheshimiana ni nguzo muhimu katika utendaji kazi wa Wizara, na kuwataka watumishi kuendeleza umoja huo hata nje ya mazingira ya kazi.
Nao baadhi ya watumishi wa Wizara wameushukuru uongozi wa Wizara ukiongozwa na Waziri Dkt. Gwajima kwa kuandaa tukio hilo na kuomba kuwa tukio hilo liwe endelevu huku wakieleza kuwa limechangia kuimarisha mshikamano, ari ya kazi na moyo wa pamoja katika kutimiza majukumu ya Wizara.
Hafla hiyo imewakutanisha watumishi wote wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kufurahi pamoja, kubadilishana uzoefu, uzoefu na kuimarisha mahusiano ya kikazi. Aidha, watumishi walipata fursa ya kushiriki chakula cha jioni na burudani mbalimbali zilizoandaliwa maalum kwa ajili ya tukio hilo.








No comments:
Post a Comment