TANZANIA IMEIMARISHA MAENDELEO NA HAKI ZA KIJAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, February 7, 2026

TANZANIA IMEIMARISHA MAENDELEO NA HAKI ZA KIJAMII



Na Mwandishi Wetu WMMJW-New York Marekani


Tanzania chini ya uongozi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maendeleo ya jamii na haki za kijamii yameimarika na kuwa kati ya vipaumbele vya Ajenda ya Kitaifa inayojumuishwa katika mfumo wa kisera na kisheria wa nchi ikiwa ni pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na utekelezaji wake ukinyumbulishwa katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050 ambayo pia huakisi utekelezaji wa Ajenda za kikanda na kimataifa kama Maendeleo Endelevu 2030.

Hayo yamesemwa katika Kikao cha 64 cha Tume ya Maendeleo ya Jamii (CSocD64) na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye Kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon A. Mpanju, wakati wa Kikao hicho kinachofanyika jijini New York nchini Marekani kuanzia tarehe 2 Februari 2026 na kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 10 Februari 2026.

Wakili Mpanju amesema amesema Tanzania inaendeleza sera zenye kuratibiwa vyema katika ukuaji wa uchumi na Ulinzi wa Jamii, maendeleo ya rasilimali watu, na upatikanaji sawa wa huduma za msingi. Juhudi hizo zinaimarishwa na sera za kisekta zinazoendana na ulinzi wa jamii, usawa wa kijinsia, maendeleo ya vijana, elimu, afya, na ulinzi wa makundi maalum hususan Wanawake,Wazee,Watoto na watu wenye ulemavu sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu namba (SDGs) 1, 5, 8, 10, na 16.

Wakili Mpanju ameeleza kuwa katika ulinzi wa kijamii Tanzania imeongeza wigo kwa kiasi kikubwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambapo katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 zaidi ya wanufaika milioni 1.26 wamefikiwa wakiwakilisha kaya zote maskini zilizotambuliwa, ambapo walengwa walipokea ruzuku za fedha. Hatua hizi zimeimarisha usalama wa kipato cha kaya, kuboresha upatikanaji wa huduma za elimu na afya, na kuongeza uhimilivu dhidi ya mishtuko ya kiuchumi na changamoto za tabianchi.

Aidha, ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua katika usawa wa kijinsia, uwezeshaji vijana na ushirikishwaji wa jamii ambapo Ushiriki wa wanawake katika uongozi na maamuzi umeendelea kuongezeka katika mihimili na ngazi mbalimbali za kiutawala za serikali mathalani idadi ya wabunge kwenye Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania imeongezeka na kufikia 40.5%. Suala hili la ongezeko la idadi ya wanawake imechagizwa na uwepo wa mipango na bajeti zenye mlengo wa jinsia ambapo kupitia mpango wa 10% wa Mikopo ya Mapato ya Ndani ya kila Halmashauri, mikopo isiyo na riba inaendelea kutolewa kwa wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na shughuli ndogo za kiuchumi.

Pia wmesisitiza kuwa katika sekta ya elimu, Serikali imeendelea kutekeleza elimu ya msingi bila malipo ambayo imechangia ongezeko la uandikishaji watoto hususan katika elimu ya msingi. Kupitia Mpango huo, zaidi ya watoto milioni mbili wakiwemo watoto 3,200 wenye mahitaji maalum waliandikishwa. Katika kuimarisha ujuzi na ustadi serikali imewekeza katika vyuo vya ufundi stadi ambapo usajili katika ngazi hiyo umepanda kwa 43% ambayo ni sawa na wanafunzi 265,000 kwa mwaka 2025/26. Sambamba na utekelezaji huo program za mafunzo kwa walimu zimeimarishwa na kuwafikia walimu zaidi ya 300,000 nchini.

“Bajeti ya Mikopo kwa wanafunzi wa vyuo na taasisi za elimu ya juu imeongezeka kutoka Wanafunzi 149,472 mwaka 2020/2021 na kufikia Wanafunzi 245,384 kwa mwaka 2024/2025. Aidha, bajeti ya mikopo kwa elimu ya juu imeongezeka kutoka bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi bilioni 787.4 mwaka 2024/2025 hali inayotoa fursa kwa vijana wengi kupata elimu ya juu bila vikwazo.” Amesisitiza Wakili Mpamju

Akizungumzia sekta ya afya Wakili Mpanju amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kutekeleza mpango wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote ambapo Tanzania imepitisha sheria ya bima ya afya kwa wote ya mwaka 2025 na utekelezaji wake umeanza kwa serikali kutenga rasilimali fedha zitakazo wezesha utolewaji wa huduma hiyo kwa kaya zilizo katika mazingira hatarishi mfano wazee, watoto, watu wenye ulemavu na watu wenye magonjwa sugu.

“Katika eneo la miundombinu ya Afya idadi ya zahanati, vituo vya afya na hospital imeongezeka kutoka 8,549 kwa mwaka 2020 na kufikia 12,846 kwa mwaka 2025. Sambamba na hilo ajira kwa watumishi wa afya imeongezeka zaidi ya mara tatu katika kipindi hicho. Uwekezaji huu umepanua upatikanaji wa huduma nchi nzima na kuchangia kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano,vifo vya mama wajawazito na kupanua wigo wa matibabu kwa magonjwa sugu na magonjwa na yasiyoambukiza.” amefafanua Wakili Mpanju

Wakili Mpanju katika kuimarisha uchumi jumuishi Serikali imeongeza uwekezaji katika sekta za kilimo, viwanda na madini kwa kuimarisha mifumo ya uzalishaji,uongezaji wa thamani na kuimarisha masoko hali iliyopelekea ongezeko la uzalishaji wa chakula na kipato. Hili limewezekana kwa kuanzisha mashamba ya kilimo biashara,uanzishaji wa viwanda 47,000 na kuweka kongani maalum za kiuchumi na uzalishaji katika mikoa lengo likiwa kupanua wigo wa ajira na thamani ya mazao ya sekta hizi.

Akitoa Ahadi ya nchi katiak Mkutano huo Wakili amesema Tanzania itaendeleza Maendeleo ya Jamii na Haki za Jamii kupitia kupitia Sera zenye Usawa, Jumuishi na zinazoratibiwa vyema katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mashirikiano ya kimataifa hususan kwenye eneo la upatikanaji wa rasilimali fedha, tekinolojia rafiki na kujengeana uwezo katika kutimiza maazimio ya Copenhagen na Doha.

Tanzania mnamo tarehe 4 Februari 2026, imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Maazimio la Copenhagen na Mpango wa Utekelezaji wa mwaka 1995 na Doha wa mwaka 2025 yaliyopitishwa na Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo ya Jamii. Taarifa hiyo imewasilishwa katika Kikao cha 64 cha Tume ya Maendeleo ya Jamii (CSocD64) kinachoongozwa na Mada Kuu isemayo "Uendelezaji wa Maendeleo na Haki za kijamii kupitia Sera za Usawa, Jumuishi na zinazoratibiwa vyema’’.



No comments:

Post a Comment