MHE BALOZI OMAR: SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 14, 2026

MHE BALOZI OMAR: SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII



Na Benny Mwaipaja, Tanga


SERIKALI imeahidi kutoa shilingi Milioni 750 ili kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyosalia katika Kituo kipya cha Afya Kange, kilichopo katika kata ya Maweni, jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi katika kata hiyo.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi jijini Tanga ambapo alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Kituo cha Afya Maweni , mradi wa mabweni katika Shule Kongwe ya Sekondari Usagara na Mradi wa Ukarabati wa Shule Kongwe ya Msingi Funguni Wilaya ya Pangani.

“Baada ya kuwasilishwa kwa maombi ya fedha za kukamilisha ujenzi wa Kituo hiki na uongozi, nimenong’ona na Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga na Mkuu wa Wilaya na baada ya majadiliano yao wamenieleza kuwa zinahitajika shilingi milioni 750, ili majengo yote yakamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi, nitawasiliana na mkoa, Halmashauri ya Jiji na Wizara ya Fedha ili kiasi hicho kipatikane na kukamilisha ujenzi” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aliwataka wakazi wa mkoa huo kufuata maelekezo ya wataalam wa afya kupunguza maradhi kwa kutunza mazingira, kuchemsha maji ya kunywa, kusafisha maeneo ya makazi ili kuua vimelea vinavyosababisha marafhi ikiwemo kipindupindu na kwa wale watakao ugua basi wakitumie kikamilifu Kituo hicho cha Afya Kange.

Mhe. Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa wananchi kukitunza kituo hicho cha afya ili kiweze kuwafaa kwa muda mrefu

Aidha, Mhe. Balozi Omar alibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026, Serikali imejitahidi kuwekeza kwa kiasi kikubwa cha fedha katika Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

"Kwa mwaka huu wa fedha uliopita, Mkoa wa Tanga ulipangiwa kutumia Shilingi bilioni 528.1, na Serikali imewasilisha kiasi cha shilingi bilioni 487.5. Sawa na ufanisi wa asilimia 92 ya fedha zote zilizopangwa kutolewa," alisisitiza Mhe. Balozi Omar.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, aliishukuru Serikali, kwa kuipatia Wilaya yake kiasi cha shilingi bilioni bilioni 350 zilizoelekezwa kuekekeza miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za wananchi katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.

Kwa upande wao Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Mhe. Abdulrahman Shillow, Mganga Mkuu wa Jiji (DMO), Dkt. Stephen Mwandambo walieleza kuwa kituo hicho cha Maweni ni mkombozi kwa wananchi wapatao 40,740 wa kata hiyo, ambao awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za uzazi na matibabu.

​Aidha, alieleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga shilingi milioni 75 kwa ajili ya mwaka wa fedha ujao ili kukamilisha ujenzi wa baadhi ya majengo yaliyobaki, ikiwemo kuchomea taka, ukamilishaji wa jengo la upasuaji, na wodi ya wazazi, ili kuimarisha huduma katika kituo hicho.




No comments:

Post a Comment