WAFANYABIASHARA WAHIMIZWA KUONGEZA MAUZO NJE YA NCHI ILI KUPUNGUZA NAKISI YA BIASHARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 14, 2026

WAFANYABIASHARA WAHIMIZWA KUONGEZA MAUZO NJE YA NCHI ILI KUPUNGUZA NAKISI YA BIASHARA



Na Benny Mwaipaja, Horohoro, Tanga


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa wito kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji nchini kuongeza uzalishaji wenye tija na kuimarisha mauzo ya bidhaa katika masoko ya kimataifa ili kupunguza nakisi ya biashara (trade deficit) na kuongeza mchango wa sekta ya biashara katika kukuza uchumi wa Taifa.

Akizungumza wakati alipotembelea Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani cha Horohoro, mkoani Tanga, ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo, Mhe. Balozi Khamis alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato na uboreshaji wa mazingira ya biashara, bado ipo haja ya kuongeza thamani ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi ili Tanzania iweze kunufaika zaidi na biashara ya kimataifa.

Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa takwimu za biashara kupitia Kituo cha Forodha cha Horohoro zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita bidhaa zenye thamani ya takribani shilingi bilioni 748 zilipitia katika kituo hicho, lakini kati ya hizo, bidhaa zilizouzwa nje ya nchi zilikuwa na thamani ya takribani shilingi bilioni 238 pekee, wakati bidhaa zilizoingizwa nchini zilifikia thamani ya shilingi bilioni 510, hali inayoonesha kuwepo kwa nakisi kubwa ya biashara.

"Matarajio ya kila taifa ni kuuza bidhaa nyingi zaidi kuliko linazoagiza kutoka nje, Takwimu hizi zinatuonesha bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika kuongeza uzalishaji na kuimarisha mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi na Tanga ina fursa nyingi za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa, hivyo ni muhimu kuzitumia kikamilifu ili kupunguza nakisi hii," alisema Mhe. Balozi Khamis.

Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kupitia uwekezaji katika miundombinu ya forodha, mifumo ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo pamoja na kuimarisha vituo vya mipakani ili kurahisisha biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, alisema mafanikio ya ukuaji wa uchumi yanatoa msingi mzuri wa kuongezeka kwa shughuli za biashara nchini, akibainisha kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025 na unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026, jambo litakalochochea ongezeko la uzalishaji na biashara.

Kwa upande wa ukusanyaji wa mapato, Mhe. Balozi Khamis alisema Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani cha Horohoro, kimewekewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 136 katika mwaka wa fedha 2026/27, baada ya kuvuka matarajio ya mwaka uliopita kwa kukusanya shilingi bilioni 125, hivyo kutokana na mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi na biashara, Serikali ina imani kuwa lengo hilo litafikiwa, huku akibainisha kuwa kituo hicho kinachangia karibu robo ya mapato yote yaliyopangwa kukusanywa katika Mkoa wa Tanga.

“Serikali imetenga shilingi bilioni 573 katika Bajeti ya mwaka 2026/27 kwa ajili ya kuendeleza maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiwemo ununuzi wa scanners (midaki) 27 za kisasa zitakazowekwa katika vituo mbalimbali vya forodha nchini, ikiwemo Kituo cha Forodha cha Horohoro” alisema Mhe. Balozi Omar

Alieleza kuwa mchakato wa ununuzi wa vifaa hivyo tayari umeanza na unafanyika kwa kuzingatia taratibu zote za ununuzi wa umma, huku akieleza kuwa vifaa hivyo hutengenezwa kwa kuzingatia mahitaji maalumu ya kila kituo cha forodha, hivyo mchakato wake unahusisha usanifu, utengenezaji, ukaguzi wa ubora, usafirishaji na ufungaji kabla ya kuanza kutumika na uwekezaji huo utaongeza ufanisi wa ukaguzi wa mizigo, kuharakisha utoaji wa huduma, kuimarisha usalama wa mipaka na kuongeza usahihi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

"Hatununui tu vifaa vya kisasa, bali tunawekeza katika kuongeza ufanisi wa biashara, kuimarisha usalama wa nchi na kuhakikisha Serikali inapata mapato yake stahiki, ma Midaki hii itasaidia kujua kwa uhakika bidhaa zinazopita mipakani, kupunguza muda wa ukaguzi na kurahisisha biashara halali," aliongeza Mhe. Balozi Omar.

Aliwahimiza pia wafanyabiashara kuendelea kutumia Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani cha Horohoro, kufanya biashara halali na kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje, akisisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza mapato ya fedha za kigeni, kupunguza nakisi ya biashara (trade deficit) na kuimarisha uchumi wa nchi.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga mjini, Mhe. Dadi Kolimba, alisema Mkoa wa Tanga unaendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza nchini katika ukusanyaji wa mapato, ukiwa wa sita kitaifa, mafanikio ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na utendaji mzuri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na ushirikiano wa taasisi nyingine za Serikali zinazofanya kazi katika vituo vya mipakani.

Alisema Kituo cha Forodha cha Horohoro ni miongoni mwa vituo muhimu vya kiuchumi vinavyochangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita kituo hicho kilivuka lengo lake kwa kukusanya shilingi bilioni 125 dhidi ya lengo la shilingi bilioni 115. Aliongeza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na TRA kutatua changamoto zinazojitokeza, kuimarisha mazingira ya biashara na kuhamasisha uzalishaji pamoja na mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya nje ili kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kwa Upande wao Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Mcha Hassan Mcha, na Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani cha Horohoro, Bw. Shadrack Mbonea, walisema kuwa wamejipanga vyema kupambana na Magendo kwa kuimarisha doria za kimkakati kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali.

Walibainisha kuwa wataendelea kuimarisha ukaguzi wa mizigo inayoingia na kutoka nchini ili kuhakikisha wanatokomeza magendo lakini pia kuihakikisha kodi stahiki inakusanywa.

Katika Ziara hiyo Mhe. Balozi Omar aliambatana pia na, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, Makamishna na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zake.






No comments:

Post a Comment