
Na Shua Ndereka, OKULY BLOG - Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amezitaka Mamlaka zote za Nidhamu nchini, ikiwemo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira, kusimamia na kuzingatia ipasavyo Sheria, Kanuni na Taratibu katika usimamizi wa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma ili kuiepusha Serikali na hasara zisizo za lazima.
Waziri Kikwete ametoa agizo hilo leo Februari 9, 2026 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha mafunzo ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Mamlaka za Maji nchini, yanayohusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 (Marejeo ya mwaka 2023) pamoja na matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Rufaa, Malalamiko na Uwasilishaji wa Taarifa za Kiutumishi (PSCMIS).
Amesema kuwa, mafunzo hayo yameandaliwa kufuatia kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma katika usimamizi wa masuala ya Rasilimali Watu kwenye baadhi ya Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, hali iliyosababisha malalamiko na rufaa nyingi kurejeshwa upya.
Akitoa takwimu, Waziri Kikwete amesema kuwa kati ya rufaa 52 zilizopokelewa kutoka Mamlaka za Maji na kuamuliwa na Tume ya Utumishi wa Umma kupitia mikutano yake kwa kipindi cha Miaka ya Fedha 2023/2024, 2024/2025 hadi Desemba 2025, rufaa 20 sawa na asilimia 38 zilionekana kuwa na ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.
Hali hiyo ilisababisha Tume kuzirudisha rufaa hizo ili michakato ya kinidhamu ianze upya au baadhi ya warufani kufutiwa hatia na kurejeshwa kazini.
“Ukiukwaji huo umekuwa ukichelewesha kupatikana haki za watumishi kwa wakati, kutokana na mashauri yao kuanzishwa upya kwani sote tunafahamu kuwa, Haki iliyocheleweshwa, ni sawa na haki iliyonyimwa”. Amesema Kikwete
Katika hatua nyingine, Waziri Kikwete amesema Tume ya Utumishi wa Umma imejenga Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Rufaa na Malalamiko katika Utumishi wa Umma, pamoja na Uwasilishaji wa Taarifa za Kiutumishi (PSCMIS), hatua inayolenga kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia katika Tasnia ya Habari na Mawasiliano duniani.
Pia amewataka washiriki wa mafunzo hayo, kushiriki kikamilifu na kutumia mfumo huo ipasavyo kwa kuwasilisha taarifa sahihi na kwa wakati, ili kuiwezesha Tume kuzichakata na kuziwasilisha kwa Serikali kwa ajili ya kupanga na kuboresha masuala mbalimbali yanayohusu Utumishi wa Umma.
Waziri Kikwete ameeleza kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ina dhamana ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutimiza dhamira ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu, uwajibikaji na unaotoa huduma bora kwa wananchi.
Ofisi hiyo pia ina jukumu la kuisimamia na kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa ufanisi.
Akitoa neno la shukrani, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Bw. Kazimil Kanyanza, amesema wapo tayari kujifunza na kutekeleza mabadiliko ya Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.

Ameeleza kuwa, ujio wa mifumo ya kielektroniki katika utumishi utarahisisha utendaji kazi na kupunguza mzigo wa kubeba nyaraka nyingi, hali ambayo awali iliwalazimu watumishi kubeba makasha makubwa ya nyaraka, kwa sasa mamlaka hizo zitatumia teknolojia kuwasilisha taarifa mbalimbali kwa wakati.
Kikao kazi cha mafunzo ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Mamlaka za Maji nchini, kimeanza leo Februari 9 na kinatarajiwa kumalizika Februari 12, 2026, kikifanyika katika Ukumbi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Manispaa ya Morogoro, ambapo mgeni rasmi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete.

No comments:
Post a Comment