WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI SAME KUTUNZA MIUNDOMBINU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 19, 2026

WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI SAME KUTUNZA MIUNDOMBINU


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Same kutunza miundombinu inayojengwa na Serikali kwa manufaa yao.

Amesema hayo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Same- Ndungu- Mkomazi km 105, sehemu Mkomazi -Ndungu km 36 ambayo ujenzi wake unaendelea.

" Wizara ya ujenzi hakikisheni ujenzi wa barabara hii ya kimkakati unakamilika kwa viwango na kuchochea ukuaji wa shughuli za kilimo, uvuvi na utalii," amesisitiza Waziri Mkuu Nchemba.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara hiyo umegawanywa katika sehemu tatu ili kurahisisha ujenzi wake ambazo ni Gonja-Ndungu km 5.2, Ndungu-Mkomazi km 36 na Same- Mroyo km 56.8.

Eng. Kasekenya amebainisha kuwa katika kuiunganisha vizuri Wilaya ya Same kwa barabara za lami Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Ndungu-Miamba-Mwembe km 90, ili kuijenga kwa lami na hivyo kurahisisha usafiri kati ya maeneo ya milimani na tambarare.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Jefferson Nnko amesema wamejipanga kuhakikisha ujenzi wa barabara hizo unakamilika kwa ubora uliosanifiwa.

Waziri Mkuu Nchemba yuko katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kilimanjaro kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.



No comments:

Post a Comment