
Serikali imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 70 kupitia tozo, ada na ushuru mbalimbali zitokanazo na utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), na inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 2.3 mradi utakapoanza kuingia katika hatua ya uendeshaji.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema hayo tarehe 16 Februari 2026 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika mradi wa EACOP mkoani Tanga.
Mhe. Salome amesema mradi huo ambao umefikia asilimia 81 ulianza kutekelezwa mwaka 2022 na unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 1,443 pamoja na miundombinu mingine ikiwemo matenki na gati la kupakia mafuta.
Amefafanua kuwa mradi unatekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 5.649, huku Serikali ya Tanzania ikichangia dola milioni 374 sawa na asilimia 15 ya hisa.
Katika sekta ya ajira, amesema mradi umezalisha jumla ya ajira 10,000 katika kipindi cha ujenzi, ambapo asilimia 75 sawa na ajira 7,500 zimenufaisha Watanzania wenye ujuzi wa chini na kati, huku asilimia 25 sawa na ajira 2,500 zikinufaisha Watanzania katika nyanja mbalimbali za uhandisi, ujenzi wa mitambo ya umeme, mazingira n.k
Mhe. Salome ameongeza kuwa zaidi ya kampuni 200 za Kitanzania zimepata zabuni za kutoa huduma na bidhaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.325, huku barabara zenye urefu wa kilomita 304 zikiboreshwa ili kurahisisha shughuli za ujenzi na kuchochea uchumi wa wananchi.
Mhe.Salome amemshukuru, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kutekeleza mradi huo ambapo jitihada mbalimbali anazofanya zitawezesha mradi huo kukamilika julai 2026.



No comments:
Post a Comment