ZAIDI YA SHULE 390 ZAFIKIWA KUHAMASISHA WASICHANA KUPENDA SAYANSI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, February 10, 2026

ZAIDI YA SHULE 390 ZAFIKIWA KUHAMASISHA WASICHANA KUPENDA SAYANSI


Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Profesa Ladslaus Laurent Mnyone,akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi,inayotarajiwa kufanyika Februari 11, 2026 jijini Dodoma.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Zaidi ya shule 390 katika mikoa 14 nchini zimefikiwa kupitia kampeni maalum ya kuhamasisha wasichana na wanawake kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STI), ikiwa ni jitihada za kuongeza ushiriki wa watoto wa kike katika masomo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Profesa Ladslaus Laurent Mnyone, amesema kuwa takribani watoto wa kike 165,445 wamefikiwa na kunufaika na kampeni hiyo.

Amesema uhamasishaji huo umetolewa kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo semina, mafunzo shuleni pamoja na ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi.

Profesa Mnyone ameongeza kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha wasichana wanapata fursa sawa za kielimu, hususan katika masomo ya sayansi ambayo kwa muda mrefu yameonekana kutawaliwa zaidi na wanaume.

Aidha, amesema Wizara ya Elimu ipo katika maandalizi ya kuzindua programu ya Africa Educate Her iliyoasisiwa na Umoja wa Afrika, yenye lengo la kuweka na kutekeleza mikakati ya kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wasichana kielimu, ikiwemo mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia, umaskini pamoja na changamoto nyingine za kijamii na kiuchumi.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi yanatarajiwa kufanyika Februari 11, 2026, na yatafunguliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment