BMT YATOA ZAIDI YA BILIONI TANO KUIINUA MICHEZO NCHINI, TAIFA STARS NA TWIGA STARS WANUFAIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 2, 2026

BMT YATOA ZAIDI YA BILIONI TANO KUIINUA MICHEZO NCHINI, TAIFA STARS NA TWIGA STARS WANUFAIKA



Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kuinua sekta ya michezo nchini kwa kuhakikisha timu za taifa na wanamichezo mbalimbali wanapata ushiriki kamili katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza leo, Katibu Mtendaji wa BMT, Bi. Neema Msitha, amesema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya fedha, baraza hilo limetoa jumla ya fedha kiasi cha shilingi bilioni tano, milioni mia nane ishirini na tisa, laki nne elfu mia tatu tisini na tisa na hamsini na tisa kwa ajili ya kuziwezesha timu mbalimbali.

Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 zilitumika shilingi milioni mia nane kumi, laki moja sabini na tano elfu mia sita thelathini na tano, huku mwaka 2024/2025 zikitumika shilingi bilioni tatu, milioni mia nane tatu, laki tano sitini na sita elfu mia moja themanini na tano.

Aidha, hadi kufikia Januari mwaka wa fedha 2025/2026 tayari shilingi bilioni moja, milioni mia mbili kumi na tano, laki sita sitini na mbili elfu mia moja thelathini na tisa zilikuwa zimetumika.

Bi. Msitha amezitaja baadhi ya timu zilizonufaika na uwezeshaji huo kuwa ni Timu ya Taifa ya Netiboli, Pool Table, Ngumi pamoja na Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, Tanzania national football team (Taifa Stars) iliyoshiriki mashindano ya CHAN yaliyofanyika Tanzania, Kenya na Uganda Agosti 2025.

Vilevile, Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Wanawake, Tanzania women's national football team (Twiga Stars) ilishiriki mashindano ya WAFCON nchini Morocco Julai 2025, huku Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Watu Wenye Ulemavu “Amputee Football” ikishiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yaliyofanyika Burundi Septemba 2025.

Ameongeza kuwa Taifa Stars waliwezeshwa tena kushiriki mashindano ya AFCON yaliyofanyika Morocco Disemba 2025 na kufanikiwa kuingia hatua ya 16 bora — mafanikio yaliyozidi kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.

Timu nyingine zilizowezeshwa ni pamoja na Singida Black Stars, Timu ya Taifa ya Kuogelea, Timu ya Gofu ya Wanawake, Timu ya Taifa ya Paralimpiki, Timu ya Taifa ya Mpira wa Wavu, Timu ya Judo na Timu ya Taifa ya Gofu.

Katika riadha, timu ya taifa iliwezeshwa kushiriki mashindano ya Dunia yaliyofanyika Septemba 2025 jijini Tokyo, Japan, ambapo mwanariadha Alphonce Simbu alitwaa medali ya dhahabu, pamoja na kushika nafasi ya pili katika mbio za Shanghai, China Novemba 2023.

Kwa upande wa ngumi za wazi, BMT ilimwezesha bondia Grace Mwakamela ambaye aliweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanzania kutwaa medali ya fedha katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika Yaoundé, Cameroon mwaka 2023. Aidha, bondia Yusuf Changalawe alishinda medali ya fedha katika mashindano ya Afrika ya kufuzu Olimpiki yaliyofanyika Aprili 2024.

Hatua hizi zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali kupitia BMT katika kukuza vipaji, kuimarisha ushindani na kuiwakilisha Tanzania kwa heshima katika majukwaa ya kimataifa.





No comments:

Post a Comment