KIHONGOSI AIPONGEZA WIZARA YA NISHATI KWA MRADI WA UMEME JUA KAYENZE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, March 5, 2026

KIHONGOSI AIPONGEZA WIZARA YA NISHATI KWA MRADI WA UMEME JUA KAYENZE


Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi ameipongeza Wizara ya Nishati kwa utekelezaji wa mradi wa umeme jua wenye thamani ya shilingi bilioni 11 unaoingiza megawati tano (5) katika Gridi ya Taifa.

Kihongosi ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea mradi huo uliopo katika Kijiji cha Kayenze, Jimbo la Ushetu wilayani Kahama, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Shinyanga.

“Naipongeza Wizara ya Nishati kwa mradi huu wenye tija ambao ni sehemu ya vielelezo vya utekelezaji wa miradi ya nishati safi kwa ajili ya wananchi. Kupitia mradi huu tunaendelea kuona dhamira ya Serikali ya kupeleka maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Kihongosi

Aidha, amemshukuru na kumpongeza Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake yaliyowezesha kukamilika kwa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo mradi wa Julius Nyerere unaozalisha megawati 2,115 pamoja na mradi wa umeme jua wa Kishapu ambapo awamu ya kwanza imekamilika na kuanza kuzalisha megawati 50.

Kihongosi pia amempongeza Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba pamoja na viongozi wengine kwa usimamizi madhubuti unaoifanya sekta ya nishati kuwa imara na yenye utulivu, huku akisisitiza kasi ya utekelezaji wa miradi kuendelea.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Salome Makamba amesema umeme unaozalishwa katika mradi huo unaingizwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia njia ya msongo wa kilovolti 33 (33kV). Ameongeza kuwa mradi huo ulikamilika mwezi Mei 2025 na kuanza kufanya kazi mara moja.

Ameeleza pia kuwa pamoja na kusaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme, mradi huo umechangia maendeleo ya jamii kwa kujenga jengo la zahanati katika Kijiji cha Kayenze kwa gharama ya shilingi milioni 130.

Kuhusu usambazaji wa umeme katika Jimbo la Ushetu, Mhe. Salome amesema Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 136 jimboni humo, huku vitongoji takriban 100 vilivyosalia vitakuwa vimefikiwa na huduma hiyo ifikapo mwaka 2030. 

No comments:

Post a Comment