Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, amesema mageuzi ya matumizi ya teknolojia katika sekta ya ununuzi wa umma ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kujenga uchumi jumuishi unaowanufaisha wananchi wote kupitia usimamizi mzuri wa rasilimali za umma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hatua mpya ya kidijitali katika mfumo wa ununuzi wa umma, Bw. Simba alieleza kuwa ununuzi wa umma una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, hivyo ni muhimu usimamiwe kwa uwazi, ufanisi na kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Alisema kufuatia maelekezo ya Rais kuhusu mifumo ya serikali kuunganishwa na kusomana, PPRA imeendelea kuuboresha mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma unaojulikana kama NeST kwa kuanza kuunganisha na mifumo ya taasisi mbalimbali, zikiwemo benki.
Kwa mujibu wa Bw. Simba, hatua hiyo imeanza kwa kuunganisha mfumo wa NeST na mfumo wa Benki ya NMB, jambo litakalowezesha dhamana za zabuni za kibenki kuwasilishwa na kuhakikiwa moja kwa moja kwa njia ya kidijitali.
Alifafanua kuwa mzabuni atahitajika kuingiza namba ya dhamana aliyopatiwa na benki, kisha mfumo wa NeST utaipata moja kwa moja kutoka benki husika na kuiwasilisha kwa taasisi nunuzi bila kuhitaji barua za uthibitisho kama ilivyokuwa hapo awali.
Bw. Simba alibainisha kuwa utaratibu huo utaondoa uwezekano wa kughushi dhamana za kibenki, kupunguza muda wa uhakiki na kuongeza uwazi pamoja na uaminifu katika mchakato mzima wa ununuzi wa umma.
Aliongeza kuwa kuanzia mwezi Machi 2026, huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni kutoka Benki ya NMB kupitia mfumo wa NeST itaanza kutumika rasmi katika taasisi zote za umma zinazotumia mfumo huo.
Alisema katika hatua ya awali, mfumo huo utahusisha dhamana za zabuni, dhamana za utekelezaji wa mikataba pamoja na dhamana za malipo ya awali, ikiwa ni mwanzo wa matumizi mapana ya dhamana za kielektroniki nchini.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema benki hiyo inajivunia kuwa ya kwanza kuunganisha mfumo wake na NeST katika huduma ya uhakiki wa dhamana za kibenki kidijitali.
Bi. Zaipuna alieleza kuwa awali uthibitishaji wa dhamana hizo ulikuwa unachukua muda mrefu kutokana na matumizi ya nyaraka za karatasi na mawasiliano ya barua kati ya taasisi na benki.
Alisema kupitia mfumo mpya, taasisi za umma sasa zitaweza kuthibitisha dhamana hizo ndani ya muda mfupi kupitia mfumo wa NeST, hatua itakayopunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika michakato ya zabuni.
Aidha, alisisitiza kuwa ubunifu huo utasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuwa wakandarasi hawatalazimika tena kusubiri muda mrefu kupata uthibitisho wa dhamana zao.
Bi. Zaipuna aliongeza kuwa matumizi ya mfumo huo pia yatasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa kupunguza matumizi ya karatasi na usafirishaji wa nyaraka.
Alisema NMB imewekeza katika mifumo imara ya teknolojia ya habari ili kuhakikisha usalama wa taarifa na miamala ya kifedha inalindwa kwa viwango vya juu.






No comments:
Post a Comment