TANZANIA NA GHANA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MAGEUZI YA KIUCHUMI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 2, 2026

TANZANIA NA GHANA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA MAGEUZI YA KIUCHUMI.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Macho 2, 2026 amefanya mazungumzo ya pande mbili na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. John Dramani Mahama, Ikulu ndogo jijini Arusha.

Mazungumzo yao yamejikita katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Ghana, hususani katika mageuzi ya kiuchumi, ajira kwa vijana na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali za ndani badala ya kuendelea kuuza malighafi ambapo Rais Mahama ameeleza hatua zinazochukuliwa na Ghana katika kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini na kakao, kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani na kukuza uchakataji wa ndani.

Kwa upande wake Rais Dkt. Samia amesema Tanzania inaendelea kuharakisha mkakati wa uchumi wa viwanda, ikiwemo kuongeza thamani ya mazao ya kimkakati kama pamba na kuimarisha uchakataji wa madini, na kuongeza kuwa Tanzania ina nafasi muhimu ya kujifunza kutoka Ghana katika usimamizi wa rasilimali na sera za uchumi wa ndani.

Kuhusu suala la ajira kwa vijana, Marais hao wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika maendeleo ya ujuzi, ubunifu na ujasiriamali, na kusisitiza umuhimu wa kuweka mazingira bora ya uwekezaji yatakayozalisha ajira endelevu kwa vijana wa pande zote mbili.

Katika eneo la uchumi, Rais Dkt. Samia amesisitiza dhamira ya Tanzania ya kuimarisha mifumo ya fedha za kidijitali na usalama wa mitandao kama sehemu ya mkakati wa kujenga uchumi shindani na jumuishi.



No comments:

Post a Comment