Na Carlos Claudio, Dodoma.
Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma umeeleza kujivunia mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa miradi na maboresho mbalimbali yanayofanyika chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 100 za mafanikio ya Serikali.
Akizungumza Machi 5, 2026 jijini Dodoma katika viwanja vya Nyerere Square, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dodoma, Said Ibrahim, amesema taasisi hiyo imekuwa ikishiriki kikamilifu katika kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazohusiana na masuala ya vipimo.
Amesema kuwa uwepo wa taasisi hiyo katika viwanja hivyo unatokana na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ambaye alielekeza taasisi zote za umma mkoani humo kuanzisha kliniki ya pamoja kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuwapatia huduma kwa kipindi cha siku tatu sambamba na kueleza mafanikio ya Serikali katika siku 100.
“Kuanzia jana tumekuwa hapa katika viwanja vya Nyerere Square tukitoa huduma kwa wananchi. Leo tunaendelea na kesho pia tutakuwepo hapa kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao,” amesema Ibrahim.
Ameongeza kuwa wananchi wanakaribishwa kufika katika viwanja hivyo ili kuwasilisha kero zao na kupata huduma za haraka, huku akieleza kuwa kwa changamoto zinazohitaji huduma nje ya eneo hilo, maofisa wa Wakala wa Vipimo wapo tayari kufika moja kwa moja mahali alipo mwananchi na kutoa huduma stahiki.
Katika kueleza mafanikio ya siku 100 za Rais Samia, Ibrahim amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Vipimo imefanikiwa kuingia makubaliano na Wakala wa Vipimo wa Serikali ya Zambia kwa ajili ya kushirikiana katika uhakiki wa matenki pamoja na malori yanayobeba mafuta.
Amesema makubaliano hayo yamewezesha pande zote mbili kutumia mfumo unaofanana wa vipimo kwa kutumia kifaa cha dipstick katika uhakiki wa matenki ya mafuta.
“Hapo awali upande wa Zambia walikuwa wanatumia vipimo vingine tofauti na dipstick, hali ambayo ilikuwa inaleta usumbufu kwa madereva na wafanyabiashara wanaosafirisha mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia. Sasa kero hiyo imetatuliwa baada ya kufikia makubaliano hayo,” amefafanua.
Aidha, ametoa wito kwa vijana na wananchi wenye ujuzi katika masuala ya vipimo kutumia fursa iliyopo nchini Zambia kwa kwenda kufanya kazi zinazohusiana na sekta hiyo ili kujiongezea kipato na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.
Amesema ushirikiano huo wa kikazi kati ya Tanzania na Zambia ni hatua muhimu katika kurahisisha biashara ya mafuta katika ukanda huo na kuongeza ufanisi katika sekta ya vipimo.



















No comments:
Post a Comment