MWENGE WA UHURU WAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KIBITI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, April 26, 2026

MWENGE WA UHURU WAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KIBITI


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’oda, amezindua mradi wa majiko ya gesi 3,255 yanayouzwa kwa bei ya ruzuku kwa wananchi wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, ikiwa ni jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mradi huo unatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi nchini ifikapo mwaka 2034, sambamba na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwang’oda amesema matumizi ya nishati safi ni muhimu katika kulinda afya za wananchi na mazingira, akibainisha kuwa Mwenge wa Uhuru umefurahishwa na hatua hiyo.

“Ni muhimu kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda afya zetu na mazingira yetu,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi wa REA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Elvia Kazoba, amesema wananchi wa Kibiti watakuwa mfano mzuri katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Ameeleza kuwa serikali imetoa ruzuku ya asilimia 50, ambapo wananchi wataweza kununua mtungi wa gesi kwa shilingi 17,500 pekee.
Nao wafanyabiashara wa chakula maarufu kama mama lishe na baba lishe wamepongeza mradi huo wakisema utasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara zao.

Mmoja wa wafanyabiashara hao amesema awali alikuwa akitumia shilingi 33,300 kwa siku kununua mkaa, lakini kwa sasa anatumia gesi inayomwezesha kudumu hadi siku tano katika biashara yake.

“Matumizi ya nishati safi yanasaidia kutunza fedha na kuweka akiba kwenye mahitaji mengine muhimu,” amesema.

Mradi huo unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu katika kupunguza gharama za maisha, kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi.






No comments:

Post a Comment