
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imeweka wazi mkakati mpana wa mageuzi ya utumishi wa umma unaolenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupambana kwa nguvu zote na rushwa, huku ikiidhinisha ajira mpya zaidi ya 43,000 na kuimarisha mifumo ya kidijitali serikalini.
Hatua hiyo imebainishwa Aprili 17, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2026/27 ya Ofisi hiyo.
Katika hotuba yake, Waziri Kikwete alieleza mafanikio yaliyopatikana pamoja na mipango ya kuijenga Tanzania ya kisasa inayotegemea teknolojia na misingi ya utawala bora.
Amesema mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea yanahusisha matumizi makubwa ya TEHAMA, ikiwemo mifumo ya kisasa ya kuhudumia wananchi na kusimamia watumishi wa umma, hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo na kupunguza urasimu.
Katika jitihada za kupunguza uhaba wa watumishi na kuboresha utoaji wa huduma, Serikali imetoa vibali vya ajira mpya 43,866 katika taasisi mbalimbali za umma. Ajira hizo zinatarajiwa kuongeza nguvu kazi katika sekta muhimu kama afya, elimu na utawala wa umma.
Sambamba na hilo, Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara kwa maelfu ya watumishi, hatua inayotarajiwa kurejesha morali ya kazi na kuongeza ufanisi katika utendaji.
RUSHWA YABANWA
Katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 102 kupitia operesheni mbalimbali za uchunguzi nchini.
Aidha, kesi 664 zimeendeshwa mahakamani, huku Serikali ikishinda kesi 260, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha haki inatendeka na rasilimali za umma zinalindwa.
Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa wananchi, watumishi na viongozi kuhusu madhara ya rushwa kupitia mikutano, vyombo vya habari na mitaala ya elimu, ikiwa ni jitihada za kujenga jamii yenye maadili.
MAPINDUZI YA KIDIGITALI
Katika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya kidijitali.
Kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), mifumo zaidi ya 252 imeunganishwa katika mfumo wa pamoja wa kubadilishana taarifa (GovESB), hatua inayorahisisha mawasiliano kati ya taasisi za umma.
Vilevile, mfumo wa e-Mrejesho umeendelea kuwapa wananchi fursa ya kuwasilisha maoni na malalamiko yao moja kwa moja kwa viongozi, kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.
TASAF YAWAGUSA WANANCHI
Katika kupunguza umaskini, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umefanikiwa kuwafikia kaya zaidi ya 896,000 kwa kutoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 43.
Hatua hiyo imechangia kuboresha maisha ya wananchi, hususan waishio vijijini, kupitia miradi ya ajira za muda na maendeleo ya miundombinu.
UTAWALA BORA WAIMARISHWA
Serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo majengo ya ofisi, mifumo ya kumbukumbu na vituo vya TEHAMA, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa kazi serikalini.
Aidha, mafunzo mbalimbali ya uongozi na utawala bora yametolewa kwa watumishi na viongozi ili kujenga utumishi wenye weledi, uwajibikaji na matokeo chanya.
Kwa ujumla, Serikali inalenga kujenga utumishi wa umma wa kisasa, unaowajibika na unaotumia teknolojia kama nyenzo kuu ya maendeleo.
Mageuzi hayo yanakwenda sambamba na dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, ambapo utawala bora, uwazi na matumizi ya TEHAMA vinatajwa kuwa nguzo kuu za kufikia uchumi imara na shindani.

No comments:
Post a Comment