CAMARTEC YAWAINUA VIJANA KUPITIA TEKNOLOJIA ZA VIWANDANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 22, 2026

CAMARTEC YAWAINUA VIJANA KUPITIA TEKNOLOJIA ZA VIWANDANI



Na Okuly Julius ,OKULY BLOG,DODOMA


WIZARA ya Viwanda na Biashara kupitia Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) imeendelea kutoa mafunzo ya matumizi ya teknolojia za viwandani na zana za kilimo kwa vijana na wajasiriamali kwa lengo la kukuza matumizi ya teknolojia katika maendeleo ya viwanda nchini.

Hayo yameelezwa bungeni na Waziri wa wizara hiyo Mhe.Judith  Kapinga wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kapinga amesema hadi kufikia Aprili 2026, CAMARTEC kupitia Vitovu vya Teknolojia za Kihandisi (VITEKI) vya Maswa na Karatu imefanikiwa kutoa mafunzo kwa vijana 78 kuhusu matumizi ya mashine mbalimbali za viwandani.

Amesema vijana hao wamepata elimu ya kutumia mashine za kupura mazao mbalimbali ikiwemo mtama, mahindi, mbaazi na alizeti pamoja na mashine za kukamua mafuta ya alizeti.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema kupitia Kiwanda Darasa cha Kubangua Korosho cha Manyoni, vijana 16 hususan wanawake wamefundishwa namna ya kubangua na kufungasha korosho kwa viwango vinavyokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema mafunzo ya uchakataji wa siagi ya karanga yametolewa kwa wajasiriamali wanne kupitia Kiwanda Darasa cha Nzega ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza thamani ya mazao na kukuza shughuli za ujasiriamali vijijini.

Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, mafunzo hayo yana lengo la kuwawezesha wananchi kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji, kuongeza ajira na kuimarisha maendeleo ya viwanda vidogo nchini.

No comments:

Post a Comment