Na Mwandishi Wetu, Mpwapwa
Mkoa wa Dodoma, umepokea Mwenge wa Uhuru 2026 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mtera iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, ukitokea Mkoa wa Iringa.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 1,595.3 katika wilaya zote saba (7) na halmashauri nane (8) za Mkoa wa Dodoma, ambapo utapitia, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya Shilingi 23,243,056,418.58.
Dkt. Kazungu alipokea Mwenge huo kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bi. Doris Kalasa, na kueleza kuwa Mkoa wa Dodoma una miradi mikubwa ya kimkakati itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuuletea Mkoa wa Dodoma fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
“Tunamshukuru na kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuupatia Mkoa wa Dodoma rasilimali za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Miradi hii ya kimkakati imeendelea kuufungua Mkoa wa Dodoma kiuchumi, kuimarisha huduma za kijamii na kuufanya kuwa kivutio muhimu kwa uwekezaji na utalii,” amesema Dkt. Kazungu.
Aidha, ameeleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Dodoma wanathamini mchango wa Mwenge wa Uhuru katika kuhamasisha umoja, mshikamano na uzalendo miongoni mwa Watanzania.
“Katika mazingira ya amani na umoja wa kitaifa, Taifa letu linaendelea kustawi, kuvutia wawekezaji na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hakuna Taifa linaloweza kufanikiwa kiuchumi bila kuwepo kwa amani na mshikamano wa Wananchi wake,” alisisitiza.
Dkt. Kazungu ameongeza kuwa wananchi pamoja na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wameendelea kuzingatia na kutekeleza ujumbe wa kudumu wa Mwenge wa Uhuru unaohimiza uzalendo, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya Taifa, sambamba na kaulimbiu ya mwaka huu isemayo:
“Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”











No comments:
Post a Comment