HOSPITALI YA KANDA MBEYA YAONYESHA UFANISI HUDUMA ZA KIBINGWA MAONESHO YA MBEYA CITY EXPO 2026. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 27, 2026

HOSPITALI YA KANDA MBEYA YAONYESHA UFANISI HUDUMA ZA KIBINGWA MAONESHO YA MBEYA CITY EXPO 2026.


MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica Yegela, ametembelea banda la Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) katika Maonesho ya Nne ya Biashara na Kilimo (Mbeya City Expo 2026) yanayofanyika kwenye viwanja vya lililokuwa Soko la Zamani la Uhindini Jijini Mbeya.

Akiwa bandani hapo, Bi. Yegela amejionea namna wataalamu wa afya wanavyotoa huduma mbalimbali za kibingwa na kibobezi bila malipo kwa wananchi wanaofika kujitokeza kwenye maonesho hayo makubwa Nyanda za Juu Kusini.

Bi. Yegela ameupongeza Uongozi wa hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Godlove Mbwanji, kwa kusogeza huduma za kisasa na vipimo vya kibingwa karibu na jamii, hatua inayookoa muda na gharama kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya na mikoa jirani.

"Nimefarijika sana kuona namna hospitali yetu ya kanda ilivyojipanga vizuri kusogeza huduma hizi kubwa na muhimu hapa kiwanjani. Wananchi wasisubiri hadi wawe wagonjwa sana, waje sasa hivi kupata ushauri na vipimo kutoka kwa madaktari bingwa," alisema Bi. Yegela.

Aidha, ametoa wito kwa wakazi wote wa Mbeya na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo kuanzia sasa hadi yatakapotamatika tarehe 30 Mei 2026, ili kupata huduma bora za afya pamoja na kujifunza fursa mbalimbali za biashara na kilimo zilizopo mkoani hapo.

Amesema kuwa uwepo wa huduma hizo bure ni fursa ya kipekee ambayo haipaswi kuachwa hivi hivi na wananchi wanaojali afya zao.

Maonesho hayo ya Mbeya City Expo yameandaliwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, yakiwa na lengo la kukuza uchumi, biashara, kilimo, na uwekezaji mkoani humo.

Hadi sasa, maonesho hayo yamevutia taasisi nyingi za kiserikali na binafsi zinazotoa elimu na huduma mbalimbali kwa umma.



No comments:

Post a Comment