KAMATI YA BUNGE:SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA NI MHIMILI WA UCHUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 14, 2026

KAMATI YA BUNGE:SEKTA YA VIWANDA NA BIASHARA NI MHIMILI WA UCHUMI



Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake, huku ikizitaka kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kukuza uchumi wa taifa. Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika (picha ya kwanza), wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za wizara kupitia taasisi zake ambazo ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), Wakala wa Vipimo (WMA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA). Mwanyika amesema juhudi zinazofanywa na wizara hiyo zimeanza kuleta matokeo chanya katika kuimarisha mazingira ya biashara na uzalishaji nchini. Aidha, ameielekeza wizara kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia na hafifu zinazoingia sokoni, akieleza kuwa bidhaa hizo husababisha hasara kwa wazalishaji wa ndani na kuhatarisha afya pamoja na usalama wa watumiaji. Pia ameagiza hatua kali kuchukuliwa dhidi ya matumizi ya vipimo visivyo sahihi katika biashara, hususan lumbesa, ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na matumizi ya vipimo visivyo rasmi. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema wizara imepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika sekta ya viwanda na biashara nchini. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Ashura Katunzi, pamoja na viongozi wengine wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, wamesema wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi wa bidhaa na huduma nchini. Hatua hizo ni pamoja na kufanya operesheni maalumu za ukaguzi wa bidhaa bandia na kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi sahihi ya vipimo vinavyotambulika kisheria.

No comments:

Post a Comment