Na, Mwandishi wetu, Mapai - Msumbiji
TANZANIA imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha udhibiti wa maafa unaanzia ngazi ya chini ya jamii, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika tahadhari, maandalizi na mwitikio wa haraka pindi majanga yanapotokea.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, walipotembelea Wilaya ya Mapai iliyoko mkoa wa Gaza Nchini Msumbiji ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na Msumbiji kuhusu hatua za mapema za kukabiliana na majanga.
Amesema moja ya mambo makubwa yakujivunia ni namna mifumo ya usimamizi wa maafa ilivyoimarika kuanzia ngazi ya chini jambo linalosaidia kuongeza ufanisi na mwitikio wa haraka pindi majanga yanapotokea.
Aidha, akieleza faida ya ziara hiyo Wilayani Mapai ni kuchukua uzoefu wa namna ya kuongeza tija katika eneo la kurejesha hali na kukabiliana na maafa kwa kuwa na miradi ya kutosha inayosaidia jamii kuwa na mwendelezo wa hatua za kuchukua kabla ya majanga, huku akipongeza miradi inayotekelezwa katika eneo hilo ya ujenzi wa Vitalu nyumba vinavyotumika kwa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali ili kusaidia kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya majanga.
“Tumeshuhudia jinsi serikali ya Msumbiji ilivyojipanga kuanzia ngazi ya jamii katika kukabiliana na maafa kwa kuwa na miradi mbalimbali ikiwemo ya Vitalu nyumba.Hii ni hatua muhimu ambayo Tanzania tunaenda kuiboresha zaidi,” amesema Brig Jen.Ndagala.
Vilevile, amesema kuwa kwa upande wa Tanzania, juhudi kama hizo tayari zimeanza kuzaa matunda, ikiwemo ujenzi wa nyumba kwa waathirika wa maporomoko ya mawe na tope kutoka Mlima Hanang' mkoani Manyara, hatua iliyosaidia kurejesha matumaini kwa wananchi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Utawala wa Wilaya ya Mapai Mhe. Maria Helena Coreia Langa amepongeza ziara hiyo muhimu kwa wilaya yake kwa kuzingatia umuhimu na matokeo chanya yatakayoimarisha uhusiano ya nchi hizo mbili kwa kuzingatia lengo kuu la kubadilishana uzoefu kati ya nchi hizo mbili kuhusu hatua za mapema kabla ya majanga kutokea.
“Tutaendelea kuongeza ubunifu katika hatua za kukabiliana na maafa katika maeneo yetu kwani tumekuwa tukikubwa na vimbunga, mafuriko na ukame mara kwa mara, hii ni hatua muhimu ya kupeana uzoefu ili kuimarisha mifumo yetu na kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya majanga,” alisema Mhe. Maria
Aliongezea kuwa,hatua ya Tanzania kuja kujifunza na kupeana uzoefu imewapa darasa kwa namna Tanzania inavyoratibu maafa kwa kutumia mifumo ya TEHAMA na matumizi ya Akili Unde katika usimamizi wa shughuli za maafa.
“Ninawapongeza kwa namna mnavyoendelea kuweka mifumo thabiti ya kukabiliana na athari za majanga pamoja na mifumo ya tahadhari za mapema na ile ya uwepo wa Kituo cha Kitaifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura (EOCC) kinachorahisisha Mfumo wa Taarifa wa Usimamizi wa Maafa (e-MAAFA) hakika hii ni hatua nzuri, katika masuala yetu ya kusimamia maafa,” alieleza Mhe. Maria
Akieleza historia ya eneo la Mapai amesema limekuwa likikabiliwa na mafuriko makubwa ya mara kwa mara yanayosababishwa na mvua kubwa, vimbunga, na kuongezeka kwa maji ya mito (kama vile Mto Limpopo), ambayo mara kwa mara huiacha wilaya ikiwa imetengwa kwa kiasi kikubwa, kuharibu barabara, na kutishia usalama wa chakula wa ndani.








No comments:
Post a Comment