MAKAMU WA RAIS AONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA MAREHEMU BI SUZANA MAGUFULI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 29, 2026

MAKAMU WA RAIS AONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA MAREHEMU BI SUZANA MAGUFULI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mazishi ya Marehemu Bi. Suzana Ngolo Magufuli, ambaye ni Mama wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, yaliyofanyika Kilimani, Chato mkoani Geita.
Akitoa salamu za rambirambi mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya kumuombea Marehemu Bi. Suzana Ngolo Magufuli, Makamu wa Rais amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameguswa na msiba huo na anatoa salamu za pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huo.
Makamu wa Rais amewasihi Watanzania kumtumia marehemu Bi. Suzana Ngolo Magufuli kama kielelezo cha malezi ya watoto, malezi ya maadili na uzalendo kwa kuwafanya watoto kutanguliza maslahi ya Taifa mbele na kuwa tayari kutumikia Taifa kwa nafasi yeyote wanayopewa. Ameongeza kwamba namna bora ya kumuenzi marehemu Bi. Suzana Ngolo Magufuli ni kuiga mfano wa malezi bora na mema ya watoto.
 
Amesema msiba wa Bi. Suzana Ngolo Magufuli unafundisha kuwa alikuwa sehemu kuu ya malezi ya Hayati Rais Dkt. John Magufuli ambaye alitoa mchango mkubwa katika utumishi wa nchi yetu. Amesema kitendo cha wananchi wengi kutoa salamu za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii ni ishara ya Watanzania kuguswa na Maisha ya Hayati Magufuli ambaye alitumikia nchi kwa uzalendo wa hali ya juu.
 
Halikadhilika, Makamu wa Rais amemuelezea hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kama kiongozi aliyejitoa kutetea nchi pamoja na kuwa na utashi wa kujua wajibu wa kulea watu wengine na kuwafanya kuwa Viongozi wa Taifa baadaye. Ameongeza kwamba kujitoa na kufanya matendo mema kwaajili ya wengine ni matunda ya baadaye kwa mtu na familia yake.
 
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya familia Bw. Simon Nyahinga amesema familia hiyo inamshukuru kwa dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo mkubwa, huruma, faraja na mchango wake mkubwa aliyouonesha wakati wa kuugua kwa Bi Suzana Magufuli.  Amesema tangu kufariki kwa Hayati Dkt. John Magufuli, Rais Samia ameendelea kusimama pamoja na familia katika kipindi chote cha matibabu.
 
Aidha, amewashukuru Viongozi wakuu wa Kitaifa na Viongozi wakuu wastaafu kwa msaada waliyotoa na kuifariji familia wakati wa matibabu ya Bi Suzana Magufuli pamoja na wakati wa msiba. Pia ameishukuru Serikali kwa kubeba jukumu ya kugharamia shughuli zote za msiba huo.
 
Ibada ya kumuaga na kumuombea Marehemu Bi. Suzana Magufuli imeongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Mwanza Mhashamu Renatus Nkwande na kuhudhuriwa na Maaskofu mbalimbali, Mapadre, Viongozi mbalimbali, Viongozi Wakuu wastaafu, pamoja na wananchi mbalimbali.
 
Bi Suzana Magufuli amezikwa katika makaburi ya familia ya Magufuli , Kilimani Wilayani Chato.

No comments:

Post a Comment