Makatibu Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanaosimamia masuala ya mtangamano wamekutana katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya Mkutano Maalumu wa 60 wa Baraza la Mawaziri la EAC unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 22 Mei 2026.Kikao hicho cha Makatibu Wakuu kimepokea, kujadili na kupendekeza rasimu ya mapendekezo ya bajeti ya Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambayo itawasilishwa katika Mkutano Maalumu wa Mawaziri kwa ajili ya idhini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Stephen Patrick Mbundi, alisisitiza umuhimu wa mkutano huo, akieleza kuwa kupitishwa kwa mapendekezo hayo ya bajeti kutasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekretarieti na taasisi zake, ikiwemo uhaba wa watumishi pamoja na ulipaji wa madeni ya watoa huduma.
Aidha, Mhe. Balozi Mbundi ametoa rai kwa Nchi Wanachama ambazo bado hazijakamilisha michango yao kufanya hivyo kwa wakati, akirejea maelekezo yaliyotolewa na Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 7 Machi 2026. Katika mkutano huo, pamoja na masuala mengine, Nchi Wanachama zilielekezwa kukamilisha ulipaji wa madeni ya michango inayodaiwa na Jumuiya ili kuimarisha utekelezaji wa shughuli zake.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Said Shaibu Mussa, akiambatana watendaji mbalimbali wa Serikali, akiwemo Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Justin Kisoka, pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Sera katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt. Charles I. Kato.







No comments:
Post a Comment